Taarifa mbaya kwa mashabiki wa klabu ya Tabora United ni kwamba mshambuliaji wao Yacouba Sogne huenda akakosa mechi zilizosalia za Ligi Kuu kutokana na kusumbuliwa na majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu, kwani hivi sasa yupo Morocco kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.
Baada ya kupata majeraha, Yacouba alirudi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu yaliyochukua takribani miezi mitatu. Wakati alishaanza kupona na kuanza mazoezi kwa bahati mbaya akatonesha tena jeraha la goti na vipimo vikaonyesha ili awe fiti ni vyema akafanyiwa upasuaji wa ‘ligament’.
Hivyo akaanza safari ya kwenda Morocco wikiendi iliyopita kwa ajili ya matibabu ya upasuaji huo utakaofanywa na daktari bingwa wa matatizo hayo yanayomsumbua.
Akizungumza baada ya kufika Morocco, Yacouba alisema yupo tayari kwa matibabu kwani vipimo vimeshafanyika.
“Nimeshafika Morocco nimefanya vipimo nasubiri kupewa tarehe ya upasuaji ambayo nadhani itatoka wakati wowote kuanzia kesho,” Amethibitisha nyota huyo alipokua akizungumza na muandishi wa Habari.