YANGA WASHINDWE WENYEWE KWA MC ALGER...
Na Prince Hoza
WIKI iliyopita katika chapisho langu la MIKASI niliandika kwa "Simba washindwe wenyewe, Yanga wanahitaji dua", nahisi nilikuwa hivyo.
Lakini wiki hii na hasa leo naandika hivi "Yanga washindwe wenyewe kwa MC Alger hapo Jumamosi katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Wiki iliyopita niliandika Simba washindwe wenyewe kwa sababu walienda kucheza na timu ya Bravos de Maquiz ya Angola mchezo wa marudiano wa kombe la Shirikisho barani Afrika.
Simba walihitaji sare ili wafuzu robo fainali, matokeo ya 1-1 yaliwafanya wafikishe pointi 10 ambapo waliungana na CS Constantine ya Algeria waliokuwa na pointi kama hizo.
Bravos licha kwamba inaweza kufikisha pointi 10 sawa na wenzake wawili Simba na Constantine, lakini inazidiwa magoli na Simba, katika mchezo wa kwanza zilipokutana Simba na Bravos, Simba ilishinda 1-0 katika uwanja wa Mkapa.
Na ndio maana wiki iliyopita kwenye mchezo wa marudiano Simba walitakiwa sare tu ili wasonge mbele, Yanga nao walihitaji dua kwa sababu Yanga wamepewa mtihani mgumu wa kushinda mechi zote mbili ili waweze kufuzu.
Yanga walikuwa na kazi ngumu ya kusafiri hadi Afrika Kaskazini kuifuata Al Hilal ya Sudan ambayo imehamia kwa muda nchini Mauritania, katika mchezo huo wa marudiano wa Ligi ya mabingwa barani Afrika ilitakiwa iibuke na ushindi iwe isiwe.
Endapo Yanga isingepata ushindi kwa Al Hilal inayonolewa na kocha machachari Florent Ibenge raia wa DR Congo isingeweza kuzungumza chochote kuhusu kwenda robo fainali, lakini mwisho wa mchezo waliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kufufua matumaini ya kucheza robo fainali.
Mchezo unaofuata utachezwa Jumamosi katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam itacheza na MC Alger ya Algeria, katika mchezo huo Yanga wanatakiwa kushinda kwa idadi yoyote ya mabao hata moja bila inatosha.
Kwa kifupi Yanga washindwe wenyewe kwani Waarabu watacheza ugenini huku Yanga washindwe kutumia vema uwanja wa nyumbani, utofauti wa mechi ya kutaka kuingia robo au fainali ni tofauti na mechi ya fainali.
Yanga waliwahi kufungwa mabao 2-1 na wageni USM Alger ya Algeria mchezo wa fainali ya kwanza iliyofanyika mbele ya mashabiki wake jijini Dar es Salaam, lakini mechi hii ya kutaka kuingia robo fainali ni tofauti na ile ya fainali.
Fainali siku zote haina mwenyewe, lakini mechi ya Jumamosi Yanga washindwe wenyewe, ingawa Waarabu wanatakiwa kuvuna pointi moja tu ili waweze kufuzu robo fainali, lakini sio rahisi kama ilivyo kwa Yanga kupata ushindi wa aina yoyote.
Ushauri wangu kwa Yanga waingie uwanjani kwa taadhali huku wakiisoma vizuri MC Alger, najua Alger wataingia uwanjani kwa lengo moja la kutafuta bao la mapema ili liwadhoofishe Yanga katika mpango wao wa kupata ushindi.
Pia watafute mabao ya mapema aidha moja au mbili, siku hiyo wacheze mpira wa kasi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara ili kuwachosha, MC Alger wanategemea mipira iliyokufa kwani wana wapigaji faulo wazuri na pia wanajua kutumia mipira ya vichwa.
Lakini Yanga sio waoga kucheza na Waarabu, kwani wameshacheza na CR Belouizdad ya Algeria na kuwafunga 4-0 uwanja wa Mkapa wakati walipotakiwa kushinda idadi hiyo ya magoli baada ya kufungwa 3-0 kwenye mchezo wa kwanza.
Mwisho mechi ya Jumamosi ni mechi ya Yanga hivyo wajue kuutumia uwanja vema na waibuke na ushindi kwa njia yoyote, Simba wameweza kupata sare na kufuzu robo fainali, na Yanga nao washindwe wenyewe kufuzu robo fainali kwa matokeo ya ushindi kwenye ardhi ya nyumbani.
ALAMSIKI