Na Prince Hoza
VYOMBO vya Habari hapa nchini vilikuwa vinapiga kelele kila kukicha suala la kutaka nchi iruhusu uraia pacha ili iwe rahisi kwa nchi yetu kufaidika na wanamichezo wetu wanaoishi ughaibuni kuzisaidia timu zetu za taifa.
Vilio vilikuwa vikubwa kiasi kwamba kuliomba bunge letu tukufu la Jamhuri ya muungano wa Tanzania ili kuweza kubadili vifungu vya Sheria kwenye katiba yetu iliyopo.
Lakini licha ya kuomba sana, bunge letu tukufu likashindwa kuridhia maombi hayo huku baadhi ya wabunge wakakataa maombi hayo wakidai sababu za kiusalama.
Watanzania waliona nchi kama inachelewa katika upande wa michezo, kwani kila msimu timu zetu za taifa zinatolewa mapema katika michuano mbalimbali inayoshiriki.
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ni miongoni mwa timu zilizowaliza wengi baada ya kushindwa kwake kufuzu katika michuano iliyokuwa inashiriki, kwa mfano Stars ilishindwa kufuzu michuano ya mataifa Afrika, AFCON na kombe la Dunia.
Kushindwa kwake kufuzu, kuliwafanya wadau wa soka kulijia juu bunge letu kwakuwa baadhi ya wabunge ni wapenzi wakubwa wa soka, lakini malalamiko yao hayakusaidia kitu kwani walikataa.
Kwa maombi yetu na mwenyezi Mungu akasikia kilio chetu, timu zetu za taifa zimekuwa zikifuzu michuano mbalimbali inayoshiriki, Taifa Stars imefuzu mara tatu mfululizo fainali za AFCON.
Stars ilifuzu mwaka 2019 (Misti), 2023 (Ivory Coast) na mwaka huu ambazo zitafanyika nchini Morocco, licha ya kufuzu huko wachezaji ambao waliotusaidia kufuzu ni wazawa na wengine waliokubali kuchukua uraia wa nchi moja (Tanzania).
Kwenye katiba ya Tanzania, inakataza uraia wa nchi mbili, ambapo baadhi ya wachezaji wenyewe asili ya Tanzania walioko ughaibuni, wamechukua uraia wa nchi wanazoishi.
Lakini sio dhambi kwa mtu mmoja kuwa na uraia wa nchi zaidi ya moja, lakini kwa Mtanzania hilo haliwezekani, lengo la kutaka kuwe na uraia pacha ni kuisaidia timu yetu ya taifa, Taifa Stars ifanye vizuri na ikiwezekana kutwaa ubingwa wa Afrika.
Wenzetu mataifa mengine hasa yale yaliyopiga hatua yamekuwa yakifanya vizuri katika michuano ya Afrika na Dunia kwa ujumla, lakini Tanzania imekuwa ikiishia kufuzu.
Wanasema wachezaji wetu hawana quality ya kupambana kimataifa ikizidiwa na mataifa makubwa barani Afrika ambayo yana wachezaji wenye uraia pacha.
Naweza kusema baadhi ya Watanzania wamechoka na zuio hilo na wameamua kutumia njia nyingine ya kuwafanya wachezaji wa kigeni kutoka mataifa ya magharibi mwa Afrika kuchukua uraia wa hapa (Tanzania) ili kusudi iwe rahisi kuichezea timu ya taifa kama watahitajika.
Bahati mbaya ndani ya nchi hii kuna watu wenye kasumba na kila kitu kwao nongwa na kupinga chochote hata kama ni kizuri, wachezaji wa kigeni wamejitahidi sana kiasi kwamba hata Ligi yetu imeongezeka ubora wa viwango.
Hivi karibuni wachezaji watatu wa kigeni wa timu ya Singida Black Stars walipatiwa uraia na Idara ya Uhamiaji Tanzania, lakini kelele zikawa nyingi wakipinga wachezaji hao kupewa uraia, wakati uraia pacha ilishakataliwa na wakaona watumie njia hiyo.
Njia hiyo waliyoitumia ya kuwabadili uraia wachezaji wa Singida Black Stars ni nzuri na ilipaswa kupigwa ili Tanzania tuwe na quality ya wachezaji, kupinga sio rafiki kwa maendeleo ya timu zetu za taifa.
ALAMSIKI