Al Hilal imeshika hatma ya Yanga kucheza robo fainali
UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal umeshika hatma ya safari yao ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
-
Ofisa habari wa Yanga Ali Kamwe mechi dhidi ya Al Hilal ni fainali kwa sababu wanaichukulia kama vita kubwa kuliko vita nyingine kwa sasa.
-
Yanga wametua nchini Mauritius kwa ajili ya mchezo wao huo wa marudio wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Waarabu hao utakaochezwa Jumapili Januari 12.
-
Kamwe amesema hakuna kingine wanachokihitaji zaidi ya kupata matokeo mazuri hivyo jeshi lao lipo kamili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.
-
“Mambo mengine tuwaachie benchi la ufundi, hatutakiwi kutoa siri kwa sababu tunaenda kwenye uwanja wa vita . tumekuja kutafuta pointi tatu, huu mchezo ni muhimu na umeshika hatma yetu ya kufuzu na kucheza robo fainali.
-
“Hali ya hewa ni kawaida sio baridi, haitoathiri wachezaji. Maandalizi yako vizuri leo tunafanya mazoezi vipi vitatu asubuhi Gym, kutakuwa na zoezi la video kuwasoma wapinzani, jioni tunamaliza na uwanjani,” amesema.
-
Yanga wapo kundi A linaloongozwa na Al Hilal wenye alama 10, wakiwa wameshafuzu kwenda Robo Fainali, nafasi ya pili wapo MC Alger wenye alama tano, Yanga alama nne nafasi ya tatu huku TP Mazembe wakiburuza mkia na alama zao mbili.