Ramovic amtosa straika mpya Yanga
Kocha Miguel Gamondi alileta straika mpya na kujifua na kikosi cha timu hiyo kambini, Avic Town, akisubiri kusaini mkataba wakati huu wa dirisha dogo, lakini alichokutana nacho kwa kocha wa sasa, Sead Ramovic, huenda kikamshangaza baada ya kuchomolewa kikosini humo.
.
Straika huyo aliyepigwa chini na Ramovic ni Fahad Bayo, raia wa Uganda aliyekuwa akijifua na kikosi cha sasa wakati akiangaliwa na Gamondi aliyetimuliwa mwezi uliopita.
.
Wakati Ramovic akitua Yanga alikutana na Bayo akiendelea na mazoezi, lakini kocha huyo amewaambia mabosi wa timu hiyo, anataka mtu wa maana katika eneo hilo zaidi ya Mganda huyo kwani kwa kiwango alichonacho hana tofauti kabisa na kila Clement Mzize, Prince Dube, Jean Baleke na Kennedy Musonda wanaotumika eneo hilo.
.
Ramovic amewaambia mabosi wa Yanga hataki historia anataka mashine zenye uwezo wa kukifanya kikosi chake kuwa bora. Inaelezwa Bayo aliyetokea MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech, uzito wa mwili wake ndiyo umemfanya kocha huyo kumkataa, kwani ameonekana kibonge.