Mwaka 2024 ulikuwa mzuri kwenye soka
Na Prince Hoza
BOXING Day inamalizika hii leo baada ya jana kusherehekea X mass, nadhani mwaka 2024 unaelekea kwisha na siku kama ya leo yaani wiki ijayo itakuwa mwaka mpya.
Jumatano ijayo ni sikukuu ya mwaka mpya wa 2025, yapo mambo mazuri ambayo tumeyaona mwaka huu na pia yapo mabaya tumeyaona, lakini mazuri ni mengi tena yakufurahisha.
Kwenye mchezo wa soka ndio sehemu inayotazamwa na wengi ingawa pia kwenye mchezo wa masumbwi pia mazuri yamefanyika, bondia Hassan Mwakinyo naye ameingia kwenye rekodi ya waliofanya vizuri msimu huu.
Mwakinyo alitetea mkanda wake wa WBO kwa upande wa Afrika, hayo ni mafanikio ya nchi kama nchi, lakini mwaka huu umekuwa mzuri kwa Tanzania kwenye upande wa soka na hasa timu zetu kufuzu kwenye michuano ya Afrika.
YANGA KUFIKA ROBO FAINALI AFRIKA
Mwaka 2024 klabu ya Yanga SC kwa mara yake ya kwanza ilifanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya vilabu ya Ligi ya mabingwa Afrika, Yanga iliwagharimu miaka 25 kufika hatua hiyo baada ya kuvuka hatua ya makundi.
Mabingwa hao wa bara waliweza kuvuka makundi na kuingia robo fainali ambapo walikutana na timu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, hata hivyo Yanga iliondoshwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.
Malalamiko mengi baada ya mchezo huo baada ya Yanga kunyimwa goli la wazi lililofungwa na Stephanie Aziz Ki, lakini pia mwaka huu Yanga kwa mara nyingine ilifaulu tena kwa kutinga hatua ya makundi kwenye michuano hiyo ya Ligi ya mabingwa.
Kwa bahati mbaya mwaka 2024 unamalizika Yanga ikiwa mkiani kwenye kundi H inaloshiriki ikiwa na timu za TP Mazembe ya DR Congo, MC Alger ya Algeria na Al Hilal Omduman ya Sudan.
Kwenye kundi lake Yanga imefikisha pointi moja, lakini ina faida ya kucheza uwanja wa nyumbani mechi mbili zilizosalia huku moja ikitoka nje ya nchi, mimi sio mtabiri siwezi kujua la mwakani ila wamejitahidi hapo walipofikia.
SIMBA KUFIKA ROBO FAINALI AFRIKA
Mwaka 2024 pia ulikuwa mzuri kwa Wekundu wa Msimbazi, Simba SC ambapo ilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika, Simba ni kama wamekuwa na mwendelezo mzuri kwani hii imekuwa mazoea kwao kufika robo fainali.
Wekundu hao walikutana na Al Ahly ya Misri na wakatupwa nje, limekuwa gonjwa kwa Simba kuishia robo fainali lakini wamejitahidi na wanatakiwa kupewa kongole, mpira wa Tanzania umepanda maradufu, Simba inatajwa kuhusika.
Simba pia imefanya vizuri zaidi mwaka huu kwa kufika hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika, kwa bahati mbaya mwaka huu unaisha Simba ikiwa nafasi tatu ikifikisha pointi 6.
TIMU ZA TAIFA ZAFUZU AFCON
Mwaka 2024 ulikuwa mzuri kwa timu zetu za taifa za mpira wa miguu kwa upande wa wanaume, Taifa Stars ilifanikiwa kufuzu fainali za mataifa Afrika, AFCON zitakazowania a nchini Morocco.
Lakini pia timu ya taifa za vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys nayo ilifanikiwa kufuzu fainali za mataifa Afrika kwa U17 ambazo zitafanyika huko huko Morocco.
Kwa kifupi mwaka 2024 ulikuwa mzuri kwa timu zetu za taifa na vilabu vya Simba na Yanga, safu ya MIKASI inauaga mwaka 2024 kwa kuupa sifa na Mungu akipenda mwaka 2025 uwe mzuri kwa timu zetu zote zikiwemo za michezo mingine.
ALAMSIKI