Siasa zimemuondoa Gamondi, Yanga

Na Prince Hoza

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara, Yanga SC hivi karibuni walifanya maamuzi makubwa na ya kushitua nchi, baada ya kumfuta kazi kocha wake mkuu Miguel Angel Gamondi raia wa Argentina na msaidizi wake Moussa Ndaw raia wa Senegal.

Yanga waliamua kumfuta kazi Gamondi na msaidizi wake baada ya mwenendo mbaya walioanza nao msimu huu, kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Azam FC na cha mabao 3-1 dhidi ya Tabora United kilitosha kabisa kuwafuta kazi wakuu hao wa benchi la ufundi.

Kipigo hicho mfululizo ni cha kwanza kwao tangu walipoanza jukumu la kuiongoza timu hiyo iliyofanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Azam FC mabao 4-1 kwenye mchezo wa fainali uliofanyika uwanja wa New Amaan Stadium Zanzibar.

Tangu kuanza kwa msimu huu, Yanga imewachukua mechi ya tisa na ya kumi kupoteza, timu hiyo ilicheza mechi nane mfululizo ikipata ushindi na iliweka rekodi ya kipekee ya kutoruhusu bao hata moja kupenya kwenye nyavu zake.

Lakini mwenendo wa kikosi hicho msimu huu haukuvutia sana tofauti na msimu uliopita ambapo timu ilikuwa inacheza vizuri na ikipata ushindi mkubwa, Yanga ya msimu uliopita ilikuwa inamfunga mpinzani mabao 5 au 4.

Ikumbukwe msimu uliopita hata mtani wake Simba walifungwa mabao 5-1 na kumtimua kocha wao, ukiondoa Simba kufungwa 5, baadhi ya timu nyingine nazo zilikutana na kipigo hicho cha goli 5.

Kwa kifupi Yanga ya msimu uliopita ilikuwa moto wa kuotea mbali, mafanikio ambayo iliyapata msimu uliopita ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu bara, kombe la CRDB Cup na kufika robo fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Licha ya mwenendo wake wa kusuasua, Yanga ilikuwa kileleni huku ikimuacha nyuma mtani wake Simba kwa tofauti ya pointi 5, ratiba ngumu waliyokuwa nayo ya kucheza mechi 3 na timu za Coastal Union ya Tanga mechi ikipigwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha na dhidi ya Singida Black Stars mechi ikipigwa New Amaan Stadium Zanzibar.

Pia Yanga itarejea jijini Dar es Salaam kucheza dhidi ya Azam FC katika uwanja wa Azam Complex Chamazi, sio siri mechi hizo zote zilichezwa kwa ukaribu na Gamondi alikuwa akilalamikia ugumu wa ratiba.

Yanga iliweza kusafiri hadi Arusha na kupata ushindi mgumu wa bao 1-0 na lakimi pia ikasafiri hadi Zanzibar na kushinda 1-0, wakarejea Dar es Salaam na kufungwa 1-0 na hapo lawama zikaanza, mechi ambayo ilihitimisha safari yake nchini ni dhidi ya Tabora United ambapo Yanga ilifungwa mabao 3-1.

Binafsi mimi sijaona ubaya ambao Gamondi alistahili kufutwa kazi, kama kufungwa kwenye soka ni kawaida, na pia sio rahisi kumuondoa kwenye mwenye rekodi kubwa kama aliyonayo Gamondi.

Gamondi ni kocha mkubwa pengine hata wote waliowahi kupita Yanga, lakini ameharibiwa heshima yake yote, rekodi ya Yanga kwa Gamondi ni kuifikisha robo fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika msimu 2023/2024, lakini pia kumfunga mtani wake Simba mara 4 mfululizo.

Hajatokea kwenye wa namna hiyo tangu kuundwa klabu hiyo mwaka 1935, Gamondi ameondolewa kisiasa tena za mpira, sitaki kuziweka wazi kwani zinaweza kuleta tafrani ila kama ukiwa mpenzi wa soka elewa hivyo kwamba Gamondi kaondolewa Yanga kisiasa.

Siasa zipo nyingi sana, ndani ya Yanga kuna watu walikuwa hawampendi na walitaka aondoke hata leo, lakini ndani ya Simba nao hawakutaka kumuona, Gamondi alichukiwa na wote na yeye alilijua hilo, Gamondi alijua ipo siku atafukuzwa kwa uzuri wake alionao.

Endapo Gamondi angeendelea kusalia Yanga na akiendeleza makali yake, kwa vyovyote hapa tajiri wa klabu hiyo Gharib Said Mohamed maarufu GSM angekuwa shakani, kwani tayari alianza kuandamwa na mahasimu zake kibiashara na pia kisoka.

Zimepita kelele nyingi zikishutumu udhamini wake kwa zaidi ya timu moja jambo ambalo kikanuni sio kosa lakini ufanisi wa Gamondi umewafanya watu kuona kama Yanga inanunua matokeo jambo ambalo si kweli.

ALAMSIKI



Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA