MO amshinda Mkude kwenye kesi yao
Kiungo Jonas Mkude ameshindwa kesi aliyowasilisha dhidi ya METL, wadhamini wa klabu ya Simba, baada ya kupost picha yake akiwa na kinywaji cha mdhamini wa klabu hiyo mnamo Julai 12, 2023, siku ambayo alikuwa tayari ametambulishwa rasmi katika klabu ya Yanga.
Mkude alidai kuwa hatua hiyo ilikiuka mkataba wake na Yanga, akitaka fidia ya shilingi bilioni moja na malipo ya dola 100,000 za Kimarekani kwa madai kwamba kitendo hicho kilisababisha matatizo ya kitaalamu na kijamii.
METL ilitetea kesi hiyo ikisema mkataba wa Mkude na Simba ulikuwa bado unaendelea hadi Julai 30, 2023, hivyo kuchapisha picha hiyo kulikuwa ndani ya muda halali wa mkataba.
Pia, waliweka wazi kuwa mikataba yao ilieleza wazi wajibu wa mchezaji kutangaza bidhaa za wadhamini wakati wa muda wa mkataba. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama iliamua kuwa upande wa Mkude haukuweza kuthibitisha madai yake kisheria.
Mahakama iliamuru kesi hiyo kuondolewa, na gharama za kesi kuhamishiwa upande wa Mkude. Uamuzi huo sasa unatoa fursa kwa Simba kufungua kesi mpya kudai fidia kwa gharama walizotumia wakati wa kesi hiyo.