HONGERENI YANGA NA SIMBA KWA KUFUZU MAKUNDI
NA PRINCE HOZA
WIKIENDI iliyopita ilikuwa siku ya furaha kws Watanzania hasa baada ya wawakilishi wao Yanga SC na Simba SC kufuzu hatua ya makundi kwenye michuano ya kimataifa.
Yanga SC inashiriki michuano ya Ligi ya mabingwa barani Afrika wakati Simba SC inashiriki kombe la Shirikisho barani Afrika, timu zote hizo zilifanya vema katika mechi zake zilizofanyika kwenye viwanja vya nyumbani.
Ilianza Yanga SC ambao walikutana na mabingwa wa Ethiopia, CBE ambapo katika mchezo wa kwanza uliofanyika katika uwanja wa Abebe Bikila, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 ambalo liliwekwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Prince Dube Mpumalelo.
Yanga ambao ni mabingwa wa Tanzania bara, walipata ushindi mkubwa katika mchezo wa marudiano uliofanyika Zanzibar katika uwanja wa New Amaan Stadium, ushindi wa mabao 6-0 uliwapeleka moja kwa moja hatua ya makundi.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Clatous Chama, Clement Mzize, Stephanie Aziz Ki (mawili), Mudathir Yahya na Duke Abuye, jumla Yanga inaingia hatua hiyo ya makundi kwa jumla ya ushindi wa mabao 7-0, hongera nyingi ziende kwao kwa kutufikisha hatua hiyo.
Watani wao Simba SC nao walicheza na timu ya Al Ahlii Tripoli ya Libya, ambapo katika mchezo wao wa kwanza uliofanyika jijini Tripoli kwenye uwanja wa Taifa wa nchi hiyo, timu hizo zilienda sare tasa 0-0.
Lakini katika mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa Benjamin William Mkapa jijini Dar es Salaam, Wekundu wa Msimbazi, Simba SC waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kutinga hatua ya makundi kombe la Shirikisho barani Afrika.
Mabao ya Simba SC katika mchezo huo yaliwekwa kimiani na Kibu Denis, Leonel Ateba na Edwin Balua, ushindi huo moja kwa moja unawapeleka hatua ya makundi, hii sio mara ya kwanza kwa Simba au Yanga kufika makundi, isipokuwa mwanzo wa safari huanzia hapo.
Hatua ya makundi ni hatua moja muhimu ambayo inatoa mwangaza wa timu hatua kubwa ikiwemo kufika robo fainali, nusu fainali, fainali na kutwaa ubingwa, kwa misimu kadhaa ambayo Simba imefika hatua kubwa zaidi ni ya robo fainali pekee.
Mashabiki wake wamekuwa wakiota timu yao ikifika nusu fainali na baadaye icheze fainali au kutwaa ubingwa na kuwa pekee Tanzania kushinda ubingwa wa Afrika, Yanga SC wao wamewahi kufika fainali ya kombe la Shirikisho Afrika.
Msimu juzi timu hiyo iliweza kufika fainali na kujikuta inakutana na timu ya USM Alger ya Algeria, kwa bahati mbaya Yanga ilikosa ubingwa kwa mujibu wa kanuni, katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam, Yanga ilifungwa mabao 2-1 lakini katika mchezo wa marudiano uliofanyika Algiers Yanga ilishinda 1-0.
Kwa mujibu wa kanuni kitendo cha Yanga kufungwa mabao mawili nyumbani na kushinda goli moja ugenini kukaifanya ipoteze taji, msimu uliopita Yanga ilifika hatua ya makundi kwenye Ligi ya mabingwa Afrika na ilifanya vizuri hadi kuingia robo fainali.
Ikumbukwe Yanga ilipangwa kucheza na timu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambapo mwisho wa siku iliondoshwa kwa changamoto ya penalti baada ya sare tasa 0-0 kwenye mechi zote mbili.
Msimu huu pia imetinga hatua ya makundi hivyo watapambana kuona wanafika mbali zaidi, hata watani zao Simba SC ambao msimu uliopita walifika hatua ya makundi Ligi ya mabingwa Afrika na kuondoshwa kwa kipigo cha mabao 3-0 na Al Ahly ya Misri, msimu huu wameangukia kombe la Shirikisho Afrika na kufika hatua ya makundi.
Kwa vyovyote Simba wanataka kufika mbali ili kuwaridhisha mashabiki wake na Watanzania kwa ujumla, Simba hawataki kutolewa kwenye hatua hiyo kwani hawajawahi kufanya hivyo, na pia hawataki kutolewa robo fainali kwakuwa wamechoka kutolewa hatua hiyo hivyo wanataka kufika nusu fainali au fainali na ikiwezekana wabebe ubingwa.
ALAMSIKI