Ni wakati sahihi wa Haji Manara kurudi Simba au kwenda Singida Black Stars

Na Prince Hoza

MAISHA ya Haji Manara ndani ya klabu ya Yanga SC kwasasa si mazuri, na hiyo yote baada ya kumaliza adhabu yake aliyopewa na TFF, Manara alifungiwa mwaka 2022 kwa muda wa miaka miwili kwa kosa la kumshambulia kwa maneno makali Rais wa Shirikisho la soka nchini Wallace Karia.

Yanga SC ilikosa huduma ya Afisa Habari wake kwa kosa hilo hivyo uongozi wa klabu hiyo uliamua kuajili mtu mwingine ili kuziba nafasi ya Manara, Ali Shabani Kamwe alichukua nafasi ya Manara na akawa Afisa Habari wa klabu hiyo kongwe na kubwa hapa nchini.

Kamwe alikuwa mchambuzi wa Azam Tv, mwaka 2022 naye alianza kuhudumu kama bosi wa kitengo cha habari na moja kati ya sifa anazomiminiwa na mashabiki wa klabu hiyo ni kwamba ameliziba pengo la Manara vizuri.

Wanayanga walifurahishwa sana na Alikamwe, na katika miaka miwili aliyohudumu akabeba nao mataji kiasi kwamba kuanzia mkurugenzi wa GSM ambao ni wawekezaji wa klabu hiyo na Rais wa klabu hiyo Injinia Hersi Said kumkubali.

Hata wakati Manara ameruhusiwa na TFF baada ya kumaliza adhabu yake ya miaka miwili, imekuwa ngumu kurejea kwenye nafasi yake kwa sababu ya mema aliyofanya Kamwe, moja kati ya sifa kemkem ya Alikamwe ni kuanzisha mechi maalum ya kumpa jina mchezaji wa klabu hiyo.

Yanga ilifanikiwa sana kwa staili hiyo kwa mfano mechi dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, Yanga waliipa jina la Pacome Day, wachezaji wote wa Yanga pamoja na Alikamwe walipaka rangi nywele zao ili kufanana na Pacome.

Staili hiyo ilimfanya MVP wa Ligi Kuu NBC Tanzania bara Stephanie Aziz Ki kuendelea nayo mpaka sasa, maisha ya Manara yameshakuwa magumu kwani mategemeo yake ni kurejea kwenye nafasi yake ya Afisa Habari kama ilivyokuwa mwanzoni.

Manara aliwahi kuwa Afisa Habari kwenye klabu ya Simba SC na katika kipindi chake chote Simba ilitawala mpira wa Tanzania, Simba ilichukua mataji yote matatu ya hapa nchini kwa misimu minne mfululizo na pia ilifika robo fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Sifa kubwa ya Manara ni kujiamini kwake pale anapofikisha taarifa zake na pia anajua kuzungumzia na amejaa matani mengi, Manara anawachanganya wapinzani wake na hata Yanga wenyewe walimpenda kwa sababu hiyo na kuamua kumchukua.

Muda wake ndani ya Yanga naona umekwisha, sidhani kama Wanayanga watafurahishwa naye kwenye usemaji wa jumla kama Alikamwe, nafasi pekee wanayoamini ataiweza ni kuwa mtendaji mkuu kitengo cha hamasa ambacho kipo chini ya Alikamwe.

Sidhani kama Manara atakubali kuwa chini ya Alikamwe, nina taarifa kwamba wawili hao hawana maelewano mazuri na ndio maana siku Manara alipotangaza kurejea kwenye nafasi yake na alisubiri rukhsa ya uongozi, Alikamwe aliandika barua ya kujiuzuru.

Baadhi ya Wanayanga walikuja juu wakitaka Alikamwe aendelee na majukumu yake na ndio maana mitandao ilichafuka kwa comment za wasomaji, ushauri wangu kwa Haji Manara asikatae ofa zinazotumwa kwake kutoka kwa klabu nyingine zinazomtaka.

Itakuwa vizuri sana kama uongozi wa klabu ya Simba SC utaamua kurejea kwake na kumrudisha nyumbani, ijulikane wazi Afisa Habari ni kazi kama nyingine na haichagui timu ya kufanyia kazi, Manara anaweza kuirudisha Simba kwenye kilele cha mafanikio hata kama wakimpa cheo cha Afisa Uhamasishaji.

Manara akirejea Simba atawachanganya Yanga kwani anajua jinsi ya kuwapiga kwenye mishono wapinzani wake, Singida Black Stars ili kujitengenezea mashabiki wanaweza pia kumchukua Manara, kwani Manara ni bidhaa adimu iliyopo sokoni.

Kuendelea kubaki Yanga na kujifanya shabiki na mwanachama kama alivyonukuliwa na Rais wa klabu hiyo, si afya kwa Manara na haikubariki, Manara ndiye aliyeufanya mchezo huo kujizolea mashabiki na tunamkumbuka sana wakati ule alipokuwa katika uhasimu na Jerry Muro wa Yanga.

Ni wakati sahihi wa Manara kurudi Simba ama kutimkia Singida Black Stars, Yanga hapamfai tena, wameshindwa kumpa heshima yake ya kumrejesha kwenye nafasi yake, nashangaa sana kwa mtu kama Manara akisubiria kupewa kazi na mabosi wa Yanga, nadhani ushauri wangu watausikia na kufanyiwa kazi.

ALAMSIKI


Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA