Rais Samia geukia na mchezo wa riadha, unaipeperusha vema bendera ya Tanzania
Na Prince Hoza
#TupoNaMama katika upande wa michezo kwani mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya vizuri katika kipindi chake kifupi cha duru la kwanza la Urais wake wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Rais Samia amechukua Urais kutoka kwa mtangulizi wake Dkt John Pombe Magufuli aliyefariki mwaka 2021, sio siri tangu alipochukua kijiti amefanya mambo mazuri ya kuendeleza miradi ya maenceleo aliyoikuta ikiwemo ujenzi wa barabara, reli na bwawa la Nyerere.
Usafiri wa reli ya kisasa ya SGR imeanza kazi ambapo safari za Dar, Moro na Dodoma zimeanza huku umeme wa bwawa la Nyerere pia unatumika na barabara za mwendokasi nazo zinaendelea kujengwa.
Bila shaka Rais Samia anafanya vema itakuwa dhambi hatutamsifia kwa hilo kwani mtangulizi wake hayati Magufuli alisifiwa sana na Watanzania kutokana na kuanzisha miradi hiyo mikubwa kabla ya kufariki ikiwa miradi haijakamilika, kitendo cha mama Samia kuikamilisha anahitaji sifa kemkem.
Sifa nyingine anayostahili mama yetu Samia Suluhu Hassan ni kwenye upande wa michezo, kiongozi huyo mkuu wa nchi alipojngia madarakani aligeukia upande wa michezo hasa mchezo wa soka ambapo alianzisha kampeni yake iitwayo "goli la mama" kwa timu za Simba, Yanga na Taifa Stars.
Rais Samia aliingilia kati na kutoa tsh milioni 5 mpaka 10 kwa kila goli moja kwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika au kombe la Shirikisho kwa timu hizo za Simba na Yanga na baadaye timu ya taifa.
Tumeshuhudia Taifa Stars ikifuzu fainali za mataifa Afrika zilizofanyika nchini Ivory Coast, wakati Yanga ikifanikiwa kuingia fainali ya kombe la Shirikisho Afrika msimu juzi na pia iliingia robo fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika msimu jana.
Lakini pia Simba ikafanikiwa kuingia robo fainali mara mbili ya Ligi ya mabingwa Afrika, mchango mkubwa umetolewa na Rais Samia hivyo hatuna budi kumpongeza, Rais Samia pia alizisaidia timu za taifa mpira wa magongo na ya wanawake.
Timu ya taifa ya mpira wa magongo Tembo Worriers ilifanikiwa kufuzu fainali za kombe la dunia, pia timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Girls, timu zote hizo zilifuzu fainali za kombe la dunia ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu nchi ipate Uhuru.
Kwenye kiwanda cha michezo hasa soka Tanzania imepiga hatua kubwa sana, Ligi Kuu Tanzania bara kwa sasa inashika nafasi ya sita kwa ubora barani Afrika na tayari TFF na Bodi ya Ligi imeamua kuleta VAR ili kusaidia kuendesha ligi vizuri huku timu zikicheza bila kulalamikia maamuzi.
Lakini Rais Samia anatakiwa kuugeukia mchezo wa riadha, mchezo huo umesahaulika tena sana, ikumbukwe kuwa mchezo wa riadhaa ndio pekee ulioiletea heshima kubwa nchi ya Tanzania kuliko michezo yoyote ile.
Hata mchezo wa soka wenyewe bado haujaifikia riadha, kwani riadha imeleta medali ya shaba tena mara mbili, mashindano ya Olimpiki ambayo ni makubwa zaidi duniani yameleta medali mbili za shaba zilizoletwa na wanariadha Seleman Nyambui na Filbert Bayi.
Nakuomba Rais Samia ugeukie mchezo wa riadha kwani unasuasua, chama cha mchezo huo RT nawaona wanasuasua katika kupata fedha za maandalizi ya kuwaandaa Filbert Bayi wa baadaye huku kamati ya Olimpiki Tanzania inasuasua pia na inafikia kulumbana na RT.
Timu za Simba, Yanga na Taifa Stars bado hazijapeperusha bendera ya Tanzania kama ilivyo kwa Bayi na Nyambui, fainali za Olimpiki zinafanana na za fainali za kombe la dunia, lakini fainali za Olimpiki zinashirikisha michezo yote.
Kwenye mchezo wa soka Tanzania haijawahi kushinda medali yoyote hata ya bati, lakini riadha pekee imeitangaza vema Tanzania, lakini kuanguka kwa Tanzania kwenye mashindano ya riadha kiasi kwamba majirani zetu Kenya wakichukua nafasi yetu na kutamba kwenye mbio mbalimbali.
Mkombozi wa riadha hapa Tanzania kwasasa ni Rais Samia, binafsi naamini Rais Samia anaweza kuisaidia riadha na kuivusha juu ili iweze kuipeperusha bendera ya Tanzania, riadha wanaweza endapo wakiwezeshwa tu kama wanavyowezeshwa Simba, Yanga na Taifa Stars.
ALAMSIKI