Simba na Yanga sio timu za serikali
Na Prince Hoza
NIMEMSIKILIZA vizuri Rais mstaafu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa anazungumza na Wasafi FM kupitia kipindi cha Good Morning.
Mstaafu Kikwete nilimuelewa vema hasa pale alipoweka wazi kwamba vilabu vya Simba na Yanga- ni mali ya wananchi na si serikali kama ambavyo watu wanafahamu hivyo.
Hata mimi mwenyewe nilikuwa najua kwamba Simba na Yanga- ni timu za serikali kwakuwa zilihusika katika kugombana uhuru wa nchi hii, lakini Kikwete ametuweka wazi.
YANGA KUITWA TIMU YA CCM
Chama Cha Mapinduzi kwa kifupi CCM inatumia rangi ya kijani, njano na nyeusi ambayo pia klabu ya Yanga- SC inatumia rangi hizo hizo, mashabiki wa Yanga- hupendelea kuvaa nguo zenye rangi hizo tatu.
Lakini wanachama wa CCM nao huvaa nguo zenye rangi hizo hizo tatu, makao makuu ya Yanga- yapo Jangwani mtaa wa Twiga, Kariakoo jijiji Dar es Salaam pamepigwa rangi ya kijani, njano na nyeusi sawa na makao makuu ya CCM yaliyopo Dodoma na Dar es Salaam ofisi ndogo.
Mara nyingi timu ya Yanga- ikiwa inacheza endapo inapata goli mashabiki wake hupendelea kuitwa "CCM...CCM......CCM" hiyo ni ishara kubwa ya Wanayanga kuashiria timu yao imepata goli.
Hata kama inafungwa mahasimu wao Simba hupendelea kuwatania kwa kuwaita CCM, hiyo yote imenifanya niamini kwamba Yanga- ni timu ya serikali, kwa maana CCM ndio inayotawala nchi.
Historia ya Uhuru wa Tanganyika sasa Tanzania, baada ya kuungano na Zanzibar, Yanga- inatajwa kuhusika kwake na ndio maana timu hiyo ina chembe chembe za serikali, ni ngumu sana kuitenganisha Yanga- na serikali
Lakini Rais mstaafu Kikwete ameweka wazi kwamba tiku hizo ni za wananchi na aina uhusiano wowote na serikali, Kikwete ameenda mbali hata Simba nayo ni timu ya Wananchi.
Amesema ni ngumu vilabu hivyo kuwa za serikali, kwani serikali haina mpango wa kuzisimamia timu zao na zikafanya vizuri, kwa mfano miaka ya nyuma mashirikisho ya umma yaliwahi kumiliki timu na zikacheza Lig Kuu.
Lakini maendeleo yake hayakuwa mazuri kwani zilikuja kutelemka daraja, kwa mfano Reli ya Morogoro, Pamba FC ya Mwanza, Ushirika Moshi, RTC Kigoma, RTC Kagera na nyinginezo
Pia timu za majeshi kama JKT Tanzania, Ruvu Shooting, Polisi Dodoma, Polisi Morogoro, Tanzania Prisons na nyinginezo, ufanisi wake si mzuri na zikizidiwa na timu za wananchi za Simba na Yanga.
Rais mstaafu Kikwete ameendelea kwa kutuweka wazi kwamba hata Shirikisho la soka nchini TFF ni mali ya wananchi na si ya serikali, kiongozi mkuu wa nchi wa kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 amedai Baraza la Michezo la Taifa, (BMT) pekee ni mali ya serikali
Serikali yenyewe inasimamia sheria tu, wananchi ndio wenye timu hizo hivyo jukumu la kuweka sheria ni wao, wapo baadhi ya mashabiki wa soka nchini wanajua kwamba Yanga- ni timu ya serikali na Simba pia ya serikali.
Ukweli ni kwamba hizo ni timu zetu wananchi, timu za wananchi zipo nyingi ila nimezitaja Simba na Yanga kutokana na mazoea, hata Coastal Union na African Sports zote za Tanga ni timu za wananchi, Pan African, Ashanti, Tukuyu Star na nyinginezo ni mali za wananchi
ALAMSIKI