FREDDIE MICHAEL ATAWAUMBUA WATU HUMU!
Na Prince Hoza
0652-626627
KWA hakika kabisa hali inavyoelekea mwishoni mwa msimu huu, kuna watu watakuja kuumbuka, kuanzia wachambuzi mpaka mashabiki watakaatana wenyewe kwa wenyewe.
Hiyo yote inatokana na kauli zao wanazozitoa kwa mshambuliaji Freddie Michael Koblas raia wa Ivory Coast anayeichezea klabu ya Simba.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo la Januari mwaka huu sambamba na mshambuliaji mwenzake Jobe Omari raia wa Gambia.
Kwasasa Freddie na Jobe ni gumzo kubwa kwenye medani ya michezo hasa soka, wapo baadhi ya wadau tena wana majina makubwa wamefikia kuwabeza Freddie na Jobe huku wakiuponda uongozi wa Simba kwa kufanya usajili mbaya zaidi.
Kitendo cha Simba kuwatema washambuliaji Jean Baleke na Moses Phiri ambao walikuwa na rekodi nzuri za kufunga, kuliwaudhi wengi walioamini kwamba Jobe na Freddie wanaweza kuwazidi uwezo nyota hao.
Baleke raia wa DR Congo alijiunga na Simba akitokea TP Mazembe ya mjini Lubumbashi na Phiri raia wa Zambia aliyekuwa anaichezea timu ya Zanaco.
Simba iliamua kuwaacha washambuliaji hao kwa sababu haifanyi vizuri na ilishindwa kufikia malengo yake kwenye michuano ya kimataifa hasa Ligi ya mabingwa Afrika.
Lakini Baleke alikuwa na msimu mzuri kwenye Ligi Kuu bara ila kimataifa hakuwafurahisha Wanasimba, sawa na Phiri naye namba zake hazikuwa nzuri kimataifa ila kwenye ligi ya bara inasomeka.
Hivyo wawili hao wakaondoka na Jobe na Freddie wakatua Msimbazi, kadri siku zilivyozidi kusonga mashabiki wa Simba wakajigawa makundi mawili, wapo wanaomkataa Freddie na wapo wanaompa muda.
Baadhi ya wachambuzi nao wanamkataa Freddie wakidai Simba sio daraja lake, hata baadhi ya viongozi wa klabu hiyo nao wanamkataa Freddie tena wakiponda usajili wake na wakidharau kwamba mchezaji huyo hata Tandale anapatikana.
Hata hivyo Freddie anawajibu kwa vitendo, kwenye Ligi Kuu ameshafunga jumla ya magoli manne, moja akiifunga Yanga SC.
Freddie amekuwa na wastani mzuri wa kufunga, kwani ni mechi tatu mfululizo amefunga, Freddie ndiye mfungaji kwenye mchezo dhidi ya Ihefu (Singida Black Stars) na pia ni mfungaji dhidi ya Yanga na jana alifunga dhidi ya KVZ mchezo wa Ligi ya Muungano.
Mpaka sasa Freddie amefunga mabao tisa kwenye mashindano yote aliyocheza, wanaomkataa Freddie wajiandae kwa aibu kwani jamaa anajua kufunga na anaweza kufanya makubwa zaidi pindi atakapopewa muda
ALAMSIKI