BINGWA LIGI YA MUUNGANO KUAMBULIA MIL 50
Wakati KVZ ikiialika Simba katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Muungano leo kuanzia saa 2:15 usiku katika Uwanja wa Amaan, timu zinazoshiriki zimetangaziwa zawadi ya Sh50 milioni kwa itakayobeba ubingwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Awadh Maulid Mwita alisema jana kuwa bingwa wa mashindano hayo itaondoka na Sh50 milioni ilhali washindi wa pili watapata Sh30 milioni.
“Mwaka huu tumeanza na timu nne, lakini mwakani mipango yetu ni kuwa na timu nane nne Zanzibar na nne Bara. Kwa hiyo ndio maana tumeweka kiasi hicho cha fedha kwa mshindi,” alisema na kuongeza kwamba mwakani bingwa ataondoka na Sh100 milioni.