SIMBA INA KILA SABABU YA KUITOA AL AHLY

Na Prince Hoza


MWISHO wa Al Ahly umefika naweza kusema hivyo, mpira umebadilika sana hapa Afrika na tumejionea kwenye michuano iliyomalizika ya mataifa Afrika, AFCON iliyofanyika nchini Ivory Coast ambapo timu maarufu ziliambulia patupu. 

Lakini pia michuano hiyo tumeshuhudia miamba ya kutoka Afrika kaskazini, kwa maana timu za Kiarabu kuondoshwa mapema, mataifa makubwa kama ya Morocco, Algeria, Tunisia na Misri zilishindwa kupenya. 

Kushindwa kwa mataifa hayo, kulizifanya mataifa yasiyo na umaarufu kuibuka, hivyo ndivyo ilivyo kwa upande wa vilabu katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika na kombe la Shirikisho. 

Katika Ligi ya mabingwa, safari hii mataifa ya Waarabu hayajafua dafu na kujikuta yakiondoshwa mapema, Al Ahly na Esperance ya Tunisia ndio timu pekee zilizofanikiwa kuingia robo fainali, na mwenendo wao si mzuri.

Vilabu kama vya Pyramids ya Misri, Wydad Casablanca ya Morocco na CR Belouizdad ya Algeria ziliishia makundi. 

Sio kawaida kwa mataifa ya kiarabu kuondoshwa mapema, lakini utawala wao kwenye soka umeonekana kuyumba na kama si kuondoshwa kabisa. 

Ni maajabu makubwa kwa taifa la Tanzania kuingiza timu mbili robo fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika, Simba SC na Yanga SC zote zimefanikiwa kutinga hatua hiyo.

Miamba hiyo imeungana na TP Mazembe ya DR Congo, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Petro de Luanda ya Angola. 

Nyingine ni Esperance ya Tunisia, Al Ahly ya Misri na Asec Mimosas ya Ivory Coast, kama ilivyotokea kwenye michuano ya AFCON kule Ivory Coast ambapo mataifa ya Kiarabu ilipoanguka vibaya. 

Mataifa kama ya Algeria, Morocco, Maurtania, Tunisia na Misri ambapo yaliishia njiani, Ivory Coast na Nigeria zilicheza fainali na ukawa mwisho wa Waarabu. 

Al Ahly itakutana na Simba katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, nauona mwisho wa Ahly kama Simba itapambana kufa na kupona, Simba wasichukulie kama wanakutana na mkubwa wa soka barani Afrika, waichukulie kama Ahly timu ya kawaida na wanaweza kuiondosha. 

Wakati miamba hiyo inakwenda kukutana, rekodi inaonyesha timu hizo zimekutana mara sita katika kipindi cha misimu minne huku zote zikiwa sawa, Ahly imeshinda mara mbili na Simba pia mara mbili. 

Miamba hiyo imetoka sare mara mbili, rekodi inawabeba Ahly kwa kuifunga Simba mabao mengi zaidi.

Na pia imewahi kuiondosha Simba kwa mujibu wa sheria ya mabao ya kufunga na kufungwa, miamba hiyo ilikutana kwa mara ya 5 ilishinda mabao 5-0 na katika mchezo wa marudiano Simba ilishinda 1-0 ikumbukwe ilikuwa kwenye hatua ya makundi, pia msimu wa 2020/2021 zilikutana tena Simba ikishinda 1-0 mjini Dar es Salaam na ziliporudiana Cairo, Ahly ilishinda 1-0. Na mara nyingine zilikutana katika michuano ya African Football League (AFL) ambapo Ahly iliiondosha Simba kwa sheria ya magoli ya kufunga na kufungwa. Zilipokutana jijini Dar es Salaam zilitoka sare 2-2 na zilipokutana tena mjini Cairo zilitoka sare ya 1-1, ni wakati wa Simba kuiondosha nje Ahly, timu hizo zimeshakutana msimu wa  2018/2019.

ALAMSIKI


Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA