YANGA YAFA KIUME KWA MKAPA
Na Ikram Khamees.
Mabingwa wa soka Tanzania bara na wawakilishi pekee wa Afrika mashariki na kati katika michuano ya kimataifa Dar Young Africans, maarufu Yanga SC jioni ya leo imeanza vibaya fainali yake ya kwanza ya kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kufungwa mabao 2-1 na timu ya USM Alger ya Algeria.
Mchezo huo wa mkondo wa kwanza ulifanyika katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, timu hizo zitarudiana Jumamosi ijayo huko jijini Algiers nchini Algeria ambapo ili Yanga iweze kutwaa ubingwa inatakiwa kushinda mabao 2-0.
Aymen Mahious aliisaidia USM Alger kuongoza kwa bao la kwanza kunako dakika ya 32 kipindi cha kwanza kabla ya Fiston Mayele wa Yanga kuisawazishia timu yake bao dakika ya 82, wakati mashabiki wa Yanga wakiendelea kushangilia goli la Mayele.
USM Alger waliongeza goli la pili dakika ya 84 kupitia kwa Islam Meriji na kumaliza mchezo ikiwa mshindi, Yanga bado ina nafasi ya kushinda ugenini na kurudi na kombe, katika mchezo wa leo timu zote zilishambuliana kwa zamu ingawa wageni walionekana kucheza vizuri zaidi ya Yanga.
Hata hivyo pengo la Yanga kwa kiungo wake Mganda Khalid Aucho lilionekana dhahiri.