MAKALA. YANGA IKAFIE UWANJANI NA KUPINDUA MEZA ALGERIA

WAWAKILISHI wa Afrika mashariki na kati Dar Young Africans, maarufu Yanga SC ilianza vibaya kwenye mchezo wake wa kwanza wa fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika, baada ya kufungwa mabao 2-1 katika uwanja wake wa nyumbani wa Mkapa uliopo jijini Dar es Salaam. 

Yanga ilipokea kipigo hicho kutoka kwa USM Alger ya Algeria, hivyo itakuwa na kazi ngumu kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika Jumamosi ijayo mjini Algiers nchini Algeria. 



Mimi binafsi sina wasiwasi na Yanga hasa inapofikia kwenye hatua kama hii ambapo Yanga inahitaji kufia uwanjani na mwisho wa siku kuibuka na ushindi ikiwezekana wa mabao 2-0 au zaidi. 

Yanga inapewa sapoti kubwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amejitolea ndege ya serikali kusafirisha wachezaji wote wa timu hiyo, viongozi na mashabiki ili warudi na kombe na kuwafurahisha Watanzania. 

Ingawa mechi hiyo itakuwa ngumu na ya ushindani wa aina yake na hasa kutokana na USM Alger kuonyesha uwezo mkubwa uwanjani na inaonekana wazi kwamba wanakusudi ya kulibakiza kombe nyumbani kwao. 

Lakini ninavyoijua Yanga sidhani kama watakubali kurudi mikono mitupu na safari hii watawashangaza wengi, kama ilivyoanza msimu wa michuano hii ya kombe la Shirikisho, wawakilishi hao waliangukia kombe hilo hasa baada ya kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika ikifungwa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1. 



Yanga ilijikuta inakutana na timu ya Club Africans ya Tunisia ikianzia nyumbani jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Mkapa ambapo iliambulia sare tasa ya 0-0, mashabiki wa timu hiyo na wengine waliikatia tamaa pale ilipoenda kurudia mjini Tunis nchini Tunisia. 

Kwa maajabu, Yanga ilifanikiwa kusonga mbele na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na kufanikiwa kuingia hatua ya makundi, kwa rekodi inatosha kabisa wachezaji wa Yanga wanapaswa kupambana na hali yoyote ikiwezekana kufia uwanjani na mwisho wake kupata ushindi na kufanikiwa kurudi na kombe la Shirikisho barani Afrika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla. 

Ikumbukwe Yanga ndio timu ya kwanza nchini kuweza kupata ushindi mbele ya timu za Afrika kaskazini {Waarabu}, Yanga iliifunga 1-0 Club Africans ya Tunisia kwenye ardhi ya nyumbani kwao. 

Kwa vyovyote historia itajirudia na kuweza kubeba ubingwa mbele ya waarabu kwani sio mara ya kwanza kupata ushindi mbele yao, pia Yanga ndio timu pekee Tanzania iliyowahi kufanikiwa kubeba ubingwa nje ya nchi. 



Mabingwa hao wa Tanzania bara wamewahi kushinda ubingwa wa Klabu bingwa Afrika mashariki na kati au kombe la Kagame mwaka 1993 na 1999. 

Simba na kucheza kwake vizuri kwenye michuano ya kimataifa, hawajawahi kupata ushindi nje ya nchi mbele ya Waarabu ndani ya dakika 90 na kushinda ubingwa nje ya nchi, hii ni Yanga na hii ni mechi ya kihistoria. Mwisho kila la kheri Yanga SC. Asanteni


Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA