Familia ya Mwakalebela yadai bondia huyo hakuwa mgeni kwenye ngumi
Familia ya Bondia Ibrahim Mwakalebela aliyefariki jana Hospitalini Dodoma alikowaishwa baada ya kuanguka akipigana ulingoni, imesema Marehemu hakuwa Mchezaji mpya sana ulingoni kwani hili lilikua pambano lake la tatu.
Mwakalebela alikua akishiriki pambano la utangulizi katika pambano (Main Card) kati ya bondia Mtanzania Hassan Mwakinyo na Kuvesa Katembo kutoka nchini Afrika Kusini lililofanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma weekend iliyopita.
Mwakalebela alishindwa kuendelea na pambano katika round ya tatu na kuanguka wakati akipigana na Laurent Segubo “SEGU Jr” na kukimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambapo siku ya pili alionekana ana shida eneo la kichwani na kutakiwa kufanyiwa upasuaji.
“Tulistuka sana baada ya kudondoka nilikuwa naangalia kwenye TV lakini nashukru kwa yote na kupanda ulingoni hii ni mara ya tatu hakuwa Mgeni sana na sio mzoefu sana” ———amesema Juma Mwakalebela kaka wa marehemu Bondia Ibrahim Mwakalebela.