AUSSEMS KOCHA MPYA SIMBA
Na Saida Salum. Dar es Salaam
Klabu bingwa ya soka Tanzania Bara, Simba Sc leo imemtambulisha kocha wake mkuu Mbelgiji Patrick Winand Aussems baada ya kukubaliana kufundisha klabu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Aussems anachukua mikoba ya Mfaransa, Pierre Lechantre aliyemaliza mkataba wake baada ya kuhudumu kwa miezi sita na kuipa ubingwa wa Bara iliousotea kwa misimu minne.
Hafla ya utambulisho huo ilifanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam ukiongozwa na kaimu Rais wa klabu hiyo Salim Abdallah "Try Again" ambapo alianza kwa kumsifu kocha huyo kwa kukubali kwake kutua Simba na kumtakia kazi njema ili aweze kuwapa mafanikio.
Aussems ambaye alikuwa kocha wa Nepal ameahidi kuisaidia Simba kufika mbali kisoka, kocha huyo atasaidiwa na Masoud Djuma pamoja na kocha wa makipa Muharami Mohamed "Shilton"