YANGA NAO WAJIPANGA KUILIZA SIMBA WIKIENDI HII
Na Ikram Khamees. Dar es Salaam
Baada ya Simba kufanikiwa kuwapoka wachezaji watano ambao Yanga ilikuwa ikitaka kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao, hatimaye kamati ya usajili ya klabu hiyo iliyo chini ya mwenyekiti wake Abbas Tarimba imejipanga kujibu mapigo.
Licha kwamba Simba jana kuweka wazi kuwa itaachana na beki wake Mganda, Juuko Murushid lakini wamempeleka nchini Afrika Kusini kujiunga na Supersport, taarifa za ndani kabisa zinasema beki huyo alienda Afrika Kusini kufanya majaribio tu na anarejea kimya kimya nchini kutazama michuano ya Kagame lakini ameshafanya mazungumzo na viongozi wa Yanga.
Murushid anadaiwa atasaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na mabingwa hao wa zamani na huenda akawa miongoni mwa wachezaji wataoshiriki katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo Yanga itaumana na Gor Mahia, nafasi ya Murushid kucheza Yanga ni kubwa kwani tayari Simba wameshamsaini Paschal Wawa raia wa Ivory Coast ambaye anakuwa mrithi wa Murushid katika kikosi cha Simba