UFARANSA YAITUPA NJE ARGENTINA NA MESSI WAO HADI HURUMA
Mabingwa wa dunia wa mwaka 1998 Ufaransa jioni ya leo imefanikiwa kuingia robo fainali ya kombe la dunia baada ya kuilaza Argentina kwa mabao 4-3 mbele ya staa na nahodha wao Lionel Messi.
Mchezo ulikuwa mkali na wa kusisimua na iliwachukua dakika 13 Ufaransa kuandika bao la kuongoza lililofungwa na Antoine Griezman kwa mkwaju wa penalti kufuatia Kyilian Mbappe kuangushwa eneo la hatari.
Goli hilo halikudumu kwani Argentina walisawazisha kupitia Di Maria dakika ya 43 timu hizo hadi zinaenda mapumziko zikiwa sare, kipindi cha pili Argentina waliandika bao la pili kupitia kwa Gabriel Mercardo dakika ya 48 goli ambalo nalo halikudumu kwani Ufaransa walikomboa kupitia kwa Benjamin Pavard.
Kyilian Mbappe ambaye leo alikuwa katika kiwango bora aliweza kufunga mabao ya ushindi moja dakika ya 64 na lingine dakika 68 kabla ya Sergio Aguero hajafunga la tatu kwa upande wa Argentina dakika ya 90, mechi nyingine itapigwa saa 3 usiku kati ya Ureno na Uruguay