FUNDI WA MPIRA SHAABAN KIPRESHA, AJIKITA KWENYE UKOCHA MDAULA
Na Ayubu Mhina. Pwani
Kwa wakazi wa Mdaula kata ya Bwilingu, Chalinze wilayani Bagamoyo wanamfahamu vema kwa jina la Shaaban Hussein Kipresha akiwa kama mkufunzi wa Mdaula United.
Kipresha amewahi kulisakata kabumbu la ushindani jijini Dar es Salaam, mwenyewe anasimulia kuwa amewahi kukipiga Jah People ya Magomeni Mikumi mtaa wa Ifunda, Baghdad pia ya Makuti mtaa wa Shoka sambamba na Big Bonn ya mtaa huo huo, anadai akiwa Big Bonn amecheza na wakali kama Habib Mahadhi, Khalid Ngome, Gidion Kaburi, Dyson Abiola na wengineo lakini alipokuwa Baghdad alicheza na Godfrey Kalumbeta, Hamza Mtaalamu na Jah People amecheza na George Kavila.
Kipresha alikuwa akicheza namba nane yaani kiungo, anawakumbuka sana akina Athuman Machupa, Jabir Aziz "Stima", Shekhan Rashid na wengineo ambao anakiri aliwafunika vilivyo lakini bahati haikuwa yake na akajikuta anaangukia mtaani na sasa ni kocha wa Mdaula United ya Mdaula inayoshiriki Ligi Daraja la tatu Pwani.
Kipresha tayari amehitimu kozi ya awali ya ukocha (Priliminaly Course) mjini Morogoro na sasa ni kocha mwenye uwezo wa kukaa benchini kuziongoza timu za madaraja ya chini kama hiyo ya Mdaula United na amedai lengo lake ni kusomea zaidi ukocha ili akazinoe timu za Ligi Kuu Bara, mwenyewe anadai anataka awe kama Fred Minziro kwa ngekewa ya kuzipandisha timu Ligi Kuu na yeye anataka kuanza na Mdaula United ambapo ameapa kuipandisha daraja la pili