WAMBURA AFUNGIWA MAISHA KUJIHUSISHA NA SOKA

Na Saida Salum. Dar es Salaam

Kamati ya Maadili ilikutana tarehe 14/3/2018 kupitia shauri linalomhusu Ndugu Michael Richard Wambura, Makamu Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) ambaye anashtakiwa na Sekretarieti ya TFF kwa makosa matatu ya kimaadili.

*TUHUMA ZILIZOWASILISHWA *

Sekretarieti ya TFF iliwasilisha mbele ya Kamati mashtaka matatu (3)
ambayo ni;

1. /Kupokea/kuchukua fedha za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo
     hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za
    Maadili za TFF Toleo la 2013./
2. /Kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya JEKC
    SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume
    na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013./
3. /Kufanya vitendo vinavyoshusha Hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume
    na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015)/

MAELEZO YA KOSA

Ndugu Michael Richard Wambura alichukua fedha isivyo halali kwa kughushi
barua ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED ya kujipa mamlaka ya kulipwa
kwa kula njama na waliokuwa Viongozi Wakuu wa TFF; Rais na Katibu Mkuu
waliopita. Kitendo hiki ni kuvunja maadili na kushusha hadhi ya Taasisi
ya TFF.

SHAURI LILIVYOENDESHWA

Ndugu Wambura alipelekewa wito wa kufika mbele ya Kamati siku ya tarehe
14/3/2018 ili awasilishe utetezi kuhusu tuhuma zinazomkabili. Ndugu
Wambura alipewa hiari ya kutoa utetezi huo kwa mdomo, kutuma kwa
maandishi, kuleta mashahidi au kutuma mwakilishi kama kifungu cha 58 cha
Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013 kinavyoelekeza. Ndugu Wambura
alimtuma mwakilishi wake, Wakili Emanuel Muga, aliyefika na kuthibitisha
kuwa ametumwa na mteja wake (Ndugu Michael Richard Wambura) kuwasilisha
utetezi wake mbele ya Kamati.

Baada ya kuelezwa mashtaka yanayomkabili mteja wake, Wakili Muga
aliiomba Kamati kuwa mteja wake anaomba kupewa muda wa kupitia shauri
hilo ili aandae utetezi, vielelezo, na mashahidi. Mara baada ya kutoa
ombi hilo Kamati ilimruhusu asubiri ili ipitie kabla ya kufanya uamuzi.
Baada ya majadiliano wajumbe walikubaliana kuwa suala hili si geni kwa
Ndugu Wambura; hivyo siyo kweli kuwa hana ufahamu nalo. Pia moja ya
vielelezo vilivyowasilishwa mbele ya Kamati ni utetezi wa maandishi wa
Ndugu Wambura kuhusiana na suala hilo ulioandikwa 4/12/2017. Hivyo
Kamati ilijiridhisha kuwa Ndugu Wambura anao ufahamu wa kutosha wa suala
hilo na alikuwa na uwezo wa kufika mbele ya Kamati ili kutoa maelezo ya
ziada.

Kamati ilimjulisha Wakili Muga kuhusiana na uamuzi huo na kumtaka aanze
kujikita katika kujibu mashtaka yaliyowasilishwa mbele yake. Hata hivyo
Wakili Muga hakutaka kufanya hivyo na badala yake aliomba apewe muda
zaidi wa kuandaa utetezi, vielelezo, na mashahidi. Kamati ilimkumbusha
Wakili Muga kuwa wito wake ulijieleza vizuri hivyo ilikuwa ni wajibu
wake kumshauri mteja wake ipasavyo na kumsaidia katika kujibu mashtaka
yaliyofikishwa mbele yake. Baada ya maelezo hayo Kamati ilimuuliza
Wakili Muga kama yuko tayari kuendelea na shauri au vinginevyo na yeye
akaridhia kuwa shauri liendelee.

Baada ya makubaliano hayo, Wakili Muga alipewa nafasi ya kujibu mashtaka
matatu yanayomkabili mteja wake.

Shitaka la kwanza:

“Kupokea/kuchukua fedha za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo  hayakuwa
halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za
TFF Toleo la 2013.”

Sekretarieti iliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa Ndugu Michael
Richard Wambura alipokea malipo kutoka Chama cha Miguu Tanzania (FAT) na
baadaye TFF ikiwa ni marejesho ya mkopo ambao FAT ilikopeswa dola la
kimarekani $30,000 kutoka katika kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED kwa
ajili ya kusaidia uendeshaji wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka
2002. Mkataba wa deni hilo ulisainiwa na Ndugu Wambura akiwa Katibu Mkuu
wa FAT. Hata hivyo Kamati haikupata nyaraka wala kumbukumbu zozote zile
zinazoonyesha kuwa Ndugu Wambura alipata idhini ya kukopa kiasi hicho
cha fedha kutoka katika Kamati Tendaji ya FAT. Vilevile Kamati haikuona
uthibitisho wa kiasi hicho kupokelewa kwenye akaunti za FAT zaidi ya
Mkataba ambao ulisainiwa na Ndugu Wambura peke yake bila kuwa na shahidi
mwingine kutoka FAT kinyume na taratibu za kawaida za mikataba. Vile
vile Kamati imeshangaa ni taratibu gani zilitumika kwa taasisi kama FAT
kuchukua mkopo mkubwa kama huo kwenye kwenye kampuni hiyo badala ya
taasisi za fedha kama vile benki ambazo ndizo zinazojishughulisha na
masuala hayo.

Sekretarieti iliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa Ndugu Wambura, kwa
nyakati tofauti, alipokea jumla ya sh.84,000,000.00 kutoka FAT na
baadaye TFF kama marejesho ya mkopo kwa niaba ya kampuni ya JEKC SYSTEMS
LIMITED. Hata hivyo Kamati haikupata uthibitisho wa kisheria kutoka
kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED unaomuidhinisha Bw. Wambura kupokea
malipo ya mkopo huo kwa niaba yake zaidi ya barua Kumb. Na.
JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa kampuni hiyo. Hata
hivyo barua hiyo, licha ya kuandikwa miaka 10 baada ya Bw. Wambura
kuchukua nusu ya mkopo huo, haikuwahi kupokelewa TFF na wala haikidhi
matakwa ya kisheria ambayo ni kuwa na Power of Attorney iliyosajiliwa
kwa Msajili wa Hati na Nyaraka.

Kulingana na ushahidi uliowasilishwa na Sekretarieti malipo ya mkopo huo
yalifanyika kwa awamu ambapo mara ya kwanza Ndugu Wambura alilipwa
$15,000 alizopokea tarehe 29/4/2004. Hata hivyo Kamati ilibaini
mapungufu katika fomu hiyo kwani maombi ya kulipwa fedha hiyo yalitolewa
na Ndugu Wambura na kuidhinishwa na yeye mwenyewe, kinyume na taratibu
za fedha.

Malipo hayo ya mkopo hayakufanyika kwa kipindi cha miaka 10, chini ya
Uongozi wa Ndugu Leodgar C. Tenga, mpaka alipoondoka madarakani na
kuingia uongozi mpya chini ya Ndugu Jamal Malinzi ndipo yalipoanza
kufanyika tena. Kamati inapata mashaka juu ya uhalali wa deni na malipo
hayo kwani hakukuwa na madai wala malalamiko yoyote yaliyowasilishwa
kudai au kukumbushia deni hilo kwa kipindi chote hicho. Katika hali ya
kawaida siyo rahisi kulipa deni hilo bila kujiridhisha uhalali wake.

Shitaka la pili

“Kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya JEKC SYSTEMS
LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu
cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.”

Sekretarieti iliwasilisha nakala ya barua ya tarehe 21/6/2016 kutoka kwa
Bibi Irene W. Maganga ambaye ni  mke wa mmiliki wa kampuni ya JEKC
SYSTEMS LIMITED, Marehemu Enock Maganga na mmoja wa wasimamizi wa
mirathi ya marehemu walioteuliwa na Mahakama Kuu Dar es Salaam. Barua
hiyo inakanusha kuwa kampuni hiyo haikuwahi kupokea malipo yoyote ya
deni hilo. Hii inaonyesha kuwa Ndugu Wambura hakuwahi kupewa mamlaka ya
kupokea fedha hizo na pia hakuwahi kuziwasilisha kwa wamiliki wa kampuni
hiyo fedha alizopokea kutoka FAT na TFF. Kwa msingi huo hata uhalali wa
barua Kumb. Na. JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa kampuni
hiyo aliyoiwasilisha kuonyesha kuwa ameidhinishwa kupokea malipo hayo
unatia shaka. Ndugu Wambura hajawahi kukanusha maelezo yaliyomo kwenye
barua hiyo licha ya kupewa nafasi akiwa Makamu wa Rais wa TFF.

Shitaka la tatu:

“Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na
ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015)”/

Kamati imejiridhisha bila shaka kuwa vitendo vya Ndugu Wambura
vinashusha hadhi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF). Kitendo cha
Ndugu Wambura kuiingiza FAT na baadaye TFF katika mkopo wa $30,000 bila
kufuata taratibu zozote ni ukiukwaji mkubwa wa maadili. Vile vile
kitendo hicho kimelipaka matope shirikisho hilo mbele ya umma kwani
mambo aliyoyafanya hayaakisi ukubwa na umuhimu wa taasisi hiyo. Kwa
nafasi yake ya Makamu wa Rais, Ndugu Wambura ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Fedha na Mipango, hivyo vitendo hivyo haviendani na hadhi na majukumu ya
nafasi yake hiyo.

HUKUMU

Kosa la kwanza:

Kulingana na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la
2013, Ndugu Michael Richard Wambura, amefanya kosa la kifisadi ambalo
adhabu zake ni;

1. (i) faini isiyopungua shilingi 10,000,000.

(ii) kifungo cha cha kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka isiyopungua 5

1. Kama suala ni zito na limekuwa likijirudia rudia, kifungo cha
    kutojihusisha na mpira wa miguu maisha.

Kosa la pili:

Kwa kosa la kughushi kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili ya TFF
toleo la 2013, kinatoa adhabu ya kifungo cha cha kutojihusisha na mpira
wa miguu kwa miaka isiyopungua 5.

Kosa la tatu:

Kwa kosa la kushusha hadhi ya Shirikisho ni kwenda kinyume na Katiba ya
TFF (kama ilivyorekebishwa 2015). Hili ni kosa la kimaadili ambalo
adhabu zake zinaenda sambamba na adhabu nyingine zinazotolewa na Kanuni
za Maadili ya TFF toleo la 2013.

Baada ya kupitia shauri hili na kuridhika pasipo na shaka kuwa Ndugu
Michael Richard Wambura ametenda makosa hayo yote, Kamati imemfungia
Ndugu Michael Richard Wambura kifungo cha kutojihusisha na mpira wa
miguu maisha. Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia uzito wa kosa lake kwa
mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.

Kwa kuwa suala hili linahusisha masuala ya rushwa, Kamati inaielekeza
Sekretarieti, kwa kupitia kifungu cha 6(3) cha Kanuni za Maadili ya TFF
toleo la 2013, ilifikishe suala hili la Ndugu Michael Richard Wambura
katika vyombo vya dola ili vifanye uchunguzi. Aidha Kamati inakubaliana
na mapendekezo ya Kamati ya Ukaguzi kuwa waliokuwa viongozi wakuu wa TFF
wakati malipo hayo yanafanyika, Ndugu Jamal Malinzi (Rais) na Ndugu
Celestine Mwesigwa (Katibu Mkuu) nao waunganishwe katika uchunguzi huo.

HITIMISHO

Kamati haikupendezwa na taarifa zilizowasilishwa na Sekretarieti kuhusu
juhudi zilizofanywa na vyombo mbalimbali kuizuia isifanye kazi yake kwa
mujibu wa Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015) na Kanuni za
Maadili ya TFF toleo la 2013. Kamati inaviasa vyombo hivyo kutoingilia
mambo ya mpira wa miguu, hasa vyombo vya kimaamuzi, kwani athari zake
zinaweza kuwa kubwa kwa ustawi wa mpira wa miguu nchini.

Michael Wambura amefungiwa maisha

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA