Yanga yaifuata Majimaji kwa mwewe, yaapa kutinga robo fainali
Na Salum Fikiri Jr. Dar es Salaam
Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga Sc wanatarajia kusafiri asubuhi ya leo kuelekea mjini Songea mkoani Ruvuma ambapo kesho Jumapili watashuka uwanja wa Majimaji kucheza na wenyeji wao Majimaji Fc hatua ya 16 bora ya kombe la Azam Sports Federation Cup, maarufu FA Cup.
Msafara wa nyota wa Yanga utaingia kwa ndege mjini Songea baadaye leo ukitokea jijini Dar es Salaam ambapo pia uliwasiri mapema juzi ukitokea Victoria nchini Shelisheli ulikoenda kucheza na Saint Louis Ligi ya mabingwa barani Afrika.
Yanga ilifanikiwa kusonga mbele kwenye michuano hiyo kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 1-0 nyumbani na kutoka sare ya 1-1 ugenini, endapo Yanga ikifanikiwa kuifunga Majimaji itakuwa imeingia robo fainali, na kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya mashindano wa Yanga, Hussein Nyika, amesema wataendeleza ubabe kwa Majimaji kesho.
Yanga iliifunga Majimaji mabao 4-1 mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika uwanja wa Taifa Dar es Salaam hivyo wameapa kushinda tena, ingawa kocha msaidizi wa Majimaji, Habibu Kondo amesema hilo halitawezekana