Staa Wetu
Habibu Kiyombo: anakuja ado ado.
Na Prince Hoza
HUWEZi Kuamini ninachokiandika, ila ukweli huko hivyo, Habibu Haji Kiyombo ndiyo mwanasoka wa kwanza Tanzania Bara msimu huu kutangazwa mchezaji Bora wa mwezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Ikumbukwe kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo hiyo ya mwanasoka Bora wa mwezi wa VPL alikuwa Mzanzibar, Mudathir Yahya Khamis, Kiyombo amekuwa Mtanzania Bara wa kwanza kushinda tuzo hiyo.
Emmanuel Okwi raia wa Uganda anayekipiga Simba Sc alishinda tuzo hiyo mwezi Agosti, wakati Shafik Batambuze naye raia wa Uganda, anayekipiga Singida United akashinda Septemba.
Baada ya hapo tuzo ikaenda kwa Mzambia, Obrey Chirwa wa Yanga Sc aliyeshinda Oktoba kisha ikaenda kwa Mzanzibar, Mudathir Yahaya wa Singida United mwezi Novemba kabla ya Desemba tuzo kwenda kwa Habibu Kiyombo ambaye ni mshambuliaji wa timu ua Mbao Fc ya jijini Mwanza.
Haikuwa rahisi Kiyombo kushinda tuzo hiyo kwani aliweza kuwabwaga John Raphale Bocco "Adebayor" mshambuliaji wa Simba Sc na Bruce Kangwa mlinzi wa Azam Fc raia wa Zimbabwe.
Mchezaji huyo aliibukia Mbao Fc msimu uliopita wa 2016/17 akiichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza akiwa kama mchezaji kijana kutoka kikosi cha pili, Kiyombo amepata mafanikio makubwa msimu huu.
Mafanikio yake yametokana na msaada mkubwa anaoutoa katika timu yake hiyo hasa pale inapoumana na vigogo Simba, Yanga, Azam na Singida United, jina lake limeanza kuwa kubwa mpaka kuanza kuwindwa na vilabu hivyo vikubwa hapa nchini kutokana na umahiri wake wa kupachika mabao.
Kiyombo amekuwa na bahati nzuri ya kuzitungua Simba na Yanga anapokutana nazo, ikumbukwe mchezaji huyo alikuwa mwiba mchungu kwa Yanga Sc baada ya kuwafunga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Hata msimu uliopita Kiyombo aliiliza Yanga zilipokutana katika michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) pia akawa miongoni mwa wafungaji dhidi ya Simba katika sare ya 2-2 msimu huu.
Kiyombo alikuwa akiwaniwa na Yanga mwanzoni mwa msimu huu na pia kwenye usajili wa dirisha dogo, lakini matajiri wa Mbao Fc hawakuwa tayari kumwachilia, umahiri wa Kiyombo unatokana na kasi yake ya upachikaji mabao kwenye ligi ya msimu huu.
Mpaka sasa Kiyombo ameshafunga mabao tisa akiwa sambamba na nahodha wa Simba, John Raphael Bocco "Adebayor" ambaye naye ana mabao tisa, wote wakishika nafasi ya tatu, wakiwa nyuma ya kinara Emmanuel Okwi wa Simba Sc mwenye mabao 13 na Mzambia Obrey Chirwa wa Yanga Sc mwenye mabao kumi.
Katika mazungumzo yake, Kiyombo aliwahi kusema kuwa anatamani kuwa mfungaji bora wa msimu huu ili aweze kubeba tuzo hiyo, na kwa kasi yake ya upachikaji mabao anaweza kuibuka mfungaji bora akiwaacha nyuma wakali kama Emmanuel Okwi, Obrey Chirwa pamoja na John Bocco, Kiyombo anawaonyesha kitu Watanzania.
Bila shaka benchi la ufundi la timu ya taifa, Taifa Stars linamtizama kwa jicho pevu, sitashangaa nitakapomuona kwenye kikosi cha Stars kitakachotangazwa hapo baadaye, na kama hatojumuhishwa basi ni uamuzi mbaya kabisa kwani kwa washambuliaji bora wazalendo Kiyombo ni miongoni mwao.
Kiyombo aliyezaliwa Juni 1, 1998 anatamani pia kufikia ndoto zake za kucheza soka la kulipwa Ulaya, Kiyombo alidai anaamini uwezo wake alionao anaweza kutimiza ndoto zake hizo, hivi karibuni ilielezwa kuwa Kiyombo anafuatiliwa na klabu moja ya Ligi Kuu, Afrika Kusini.
Si kwamba mshambuliaji huyo ameanza kung' ara mwaka huu kiasi kwamba tunampigia debe aitww Taifa Stars, isipokuwa alianza kung' ara mwaka jana lakini tukashangazwa hakuitwa timu ya taifa hata ile iliyokwenda Nairobi, Kenya kushiriki michuano ya kombe la Chalenji ambapo kikosi cha Tanzania Bara kikatolewa mapema.
Kiyombo anaweza kutupa matokeo Watanzania hivyo uwepo wake kwenye timu ya taifa kwa sasa ni mkubwa, Kiyombo ameweza kuwa bora kuliko Mbaraka Yusuf ingawa naye alikuwa bora kabla hajaumia, Mbaraka amekuwa akiitwa Stars mara kwa mara.
Kuhusu timu ya Mbao Fc kufanya vibaya kwa sasa, Kiyombo amesema kuwa kukamiwa na timu pinzani kumechangia kuwakwamisha na kupata matokeo mabaya pia uchovu wa safari pia umewafanya waboronge kwani kimekuwa kikipangiwa mechi zake karibu karibu na za umbali mrefu lakini hata hivyo amesema watapigana sana kuhakikisha wanabaki Ligi Kuu Bara