STAA WETU
NI JUMA MAHADHI, KIUNGO MSHAMBULIAJI ANAYEPANDA KIWANGO NA KUSHUKA.
Na Prince Hoza
WASWAHILI husema maisha ni kupanda na kushuka, kuna wakati maisha yanakuwa fresh, na kuna wakati maisha yanabadilika na kuwa hovyo kabisa kiasi kwamba unaomba ardhi ipasuke.
Lakini hayo ndiyo maisha aliyopangiwa mwanadamu, wanasema mwanadamu furaha kwake huwa ni kidogo sana lakini shida hutawala, watu wengi wanapitia msoto huo, mmoja wapo ni kiungo mshambuliaji wa Yanga Sc, Juma Mahadhi.
Kuna wakati Mahadhi alikuwa katika kipindi kizuri sana kiasi kwamba wengi tuliamini kwamba atakuja kuwa tegemeo kwenye kikosi cha Yanga, Mahadhi alizaliwa jijini Tanga miaka 23 iliyopita na anatokea kwenye ukoo wa wanasoka.
Mahadhi ni mjukuu wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Omary Mahadhi Bin Jabir ambaye pia amewahi kuzichezea kwa mafanikio African Sports "Wanakimanumanu" ya Tanga na Simba Sc ya jijini Dar es Salaam.
Enzi zake Omary Mahadhi alisifika kwa kudaka kama nyani na ndiye aliyeiwezesha timu ya taifa ya Tanzania Bara wakati huo kutwaa kwa mara ya kwanza kombe la Chalenji mwaka 1974.
Omary Mahadhi pia aliwahi kuchaguliwa kwenye timu ya kombaini ya bara la Afrika baada ya kufanya vizuri kwenye michuano ya All Africa Games iliyofanyika nchini Nigeria, katika kikosi hicho yeye na Maulid Dilunga walikuwa Watanzania pekee kujumuhishwa kwenye kikosi hicho cha Afrika.
Huyo ndiye babu wa Juma Mahadhi wa Yanga Sc, lakini Omary Mahadhi ambaye kwa sasa ni marehemu, ameacha utitiri wa wanasoka waliotamba na wanaotamba sasa, mzee Omary Mahadhi ameacha ambapo watatu walisumbua kwelikweli kwenye soka.
Mwanaye mkubwa Rashid Mahadhi (Sasa ni marehemu) naye alirithi kipaji cha baba yake kwani alikuwa kipa aliyezichezea CDA ya Dodoma na Simba Sc ya Dar es Salaam, Rashid alifariki mwanzoni mwa mwaka huu akiwa kocha msaidizi wa Abajalo ya Sinza, watoto wengine wa mzee Mahadhi ni Habibu Mahadhi mkali wa mabao wa zamani wa Coastal Union ya Tanga.
Habibu Mahadhi amewahi kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Wakati huo ikiitwa Ligi ndogo) ikihusisha timu nane, Mahadhi alizawadiwa shilingi Milioni moja zilizotolewa na wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya bia ya TBL kupitia kinywaji chake cha Safari Lager.
Habibu pia alikuwa na mdogo wake ambaye ni Waziri Mahadhi "Mendieta" aliyekipiga kwa mafanikio Yanga Sc, Coastal Union na Moro United, katika uzao wa mzee Omary Mahadhi, Mendieta ndiye aliyekuja kung' ara kwenye soka la Tanzania pengine ndiye aliyelisimamisha jina la Mahadhi baada ya kupotea baba yao Omary Mahadhi Bin Jabir.
Sasa hivi wanaye mpwa wao ama mjukuu wa Omary Mahadhi bin Jabir, Juma Mahadhi ni mtoto wa mwanaye mzee Mahadhi ambaye ni dada wa akina Habibu, Rashid na Waziri, maisha ya Juma Mahadhi kisoka yalianzia kikosi cha pili cha Coastal Union "Wagosi wa kaya" kilichoshiriki michuano ya Uhai Cup, Mahadhi alikuwa miongoni mwa wachezaji walioisaidia Coastal Union kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, Coastal Union iliingia fainali na Yamga ambapo waliweza kushinda na kubeba kikombe.
Ilikuwa fainali nzuri ambapo kila timu ilionyesha kukamia, haikuwa rahisi Coastal kuingia fainali, kwani katika hatua ya robo fainali iliweza kuikwanyua Simba B iliyosifika kwa kucheza soka safi, Juma Mahadhi alikuwa mchezaji muhimu akifunga karibu kila mchezo hadi kuipa ubingwa timu hiyo.
Baada ya hapo akaanza kuaminiwa kwenye kikosi cha wakubwa na hasa baada ya wachezaji tegemeo kugoma, yeye na kipa wao Fikirini Hassan wakapandishwa Coastal Union na wakawa miongoni mwa wachezaji waliomalizia msimu kwenye kikosi cha kwanza.
Lakini michuano ya Copa Cocacola ndiyo iliyomuibua mpaka kunfikisha hapo halipo, zari la mentali likamuangukia Juma Mahadhi, kwani Yanga Sc wakafanikiwa kumnasa, Mahadhi alitua Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2016/17 na alijiunga na timu hiyo katika usajili wa nyongeza wa CAF.
Hakuwa peke yake katika usajili huo na hasa baada ya Yanga kufuzu hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho barani Afrika, Yanga iliongeza wachezaji wanne ambao ni Obrey Chirwa kutoka Fc Platinum ya Zimbabwe, Beno Kakolanya, Tanzania Prisons ya Mbeya pamoja na Hassan Ramadhan Kessy kutoka Simba Sc ya Dar es Salaam, Mahadhi alikuwa na wakati mzuri kwani alibahatika kusafiri na timu Uturuki ilipokwenda kuweka kambi kujiandaa na michuano hiyo na Ligi Kuu Bara.
Na maisha yalimwendea vizuri baada ya kucheza vema mchezo wake wa kwanza tena wa kimataifa dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo uwanja wa Taifa Dar es Salaam, baada ya hapo soka lake likaanza kuporomoka na maisha yakawa mabaya kwa upande wake pale Jangwani, Mahadhi aliomba ardhi ipasuke.
Benchi na yeye ni sawa na uji na mgonjwa, kilichozidi kumponza zaidi ni pale alipopaisha penalti wakati Yanga ilipocheza na Simba kuwania Ngao ya Jamii uwanja wa Taifa Dar es Salaam, katika mchezo huo Simba ilishinda kwa penalti 5-4 baada ya sare tasa ya 0-0 ndani ya dakika 90.
Safari hii Juma Mahadhi amerejea upya, maisha kwake sasa yameanza kuwa fresh, tayari alishawaomba msamaha Wanayanga kule Zanzibar ilipofanyika michuano ya kombe la Mapinduzi, Mahadhi alifunga goli na kupiga goti huku akiinama kuashiria kuomba msamaha, na baada ya hapo ameanza kucheka na nyavu kwani pia amehusika kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Saint Louis ya Shelisheli mchezo wa Ligi ya mabingwa barani Afrika, na kwa bahati mbaya Mahadhi alikosekana katika mechi ya marudiano iliyofanyika juzi uwanja wa Linite mjini Victoria ambapo timu hizo zilifungana 1-1 huku Yanga ikifuzu raundi ya pili na sasa itakutana na wawakilishi wa Botswana Township Rollers
Alamsiki