STAA WETU
: NI ASANTE KWASI, ANAYETEMBEA NA UBINGWA WA SIMBA.
Na Prince Hoza
Simba Sc ina muunganiko mzuri kuanzia sehemu ya ulinzi, kiungo hadi ushambuliaji, na hiyo ndiyo imeifanya klabu hiyo iliyozaliwa mwaka 1936 kuongoza ligi kwa tofauti kubwa ya pointi baina yake na wanaomfuatilia.
Kasi ya Simba imezidi kuongezeka katika mzunguko wa pili, Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 42 ikicheza mechi zake 18 pamoja na ule wa jana dhidi ya Mwadui Fc ulioisha kwa sare ya 2-2 uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Vinara hao wamewaacha mbali wapinzani wake Yanga, Azam na Singida United ambao wanawafuatilia kwa nyuma, kikosi hicho kinachonolewa na Mfaransa, Pierre Lechantre na msaidizi wake Masoud Djuma raia wa Burundi kimeonekana kuwa imara msimu huu na kinaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Chachu ya ushindi iliyopo katika klabu ya Simba haiji bure isipokuwa inatokana na ushirikiano mkubwa uliopo kwa wachezaji wa kikosi hicho, miongoni mwa wachezaji tegemeo ni Asante Kwasi raia wa Ghana.
Anapokosekana Kwasi, Simba inapungua makali kama ilivyotokea jana ilipokubali sare ya 2-2 na vijana wa Mwadui, Kwasi ni chaguo la Simba msimu huu akisajiliwa wakati wa usajili wa Dirisha dogo la Desemba mwaka jana, Kwasi ni beki mwenye uwezo wa kucheza pembeni na katikati, lakini pia anaweza kucheza kama kiungo mkabaji au mshambuliaji.
Alianza kufahamika msimu uliopita alipokuwa anaichezea Mbao Fc ya jijini Mwanza, Kwasi alikuwa mmoja wa wachezaji walioipa kiburi timu hiyo ambayo iliweza kuzivimbia Simba na Yanga, timu hiyo pia iliweza kuingia fainali ya kombe la Azam Sports Federation Cup na ikakutana na Simba Sc katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Kwa bahati mbaya Mbao Fc ikachapwa mabao 2-1 lakini mchezo ulikuwa mkali na wa kusisimua ulioudhuriwa na Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania,Mhe Kassim Majaliwa.
Asante Kwasi hakuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa midomoni mwa mashabiki wa soka nchini, hata vilabu vikubwa vya Yanga, Simba na Azam havikumfikiria hata kidogo, jina lililokuwa likihubiriwa sana ni la Yusuf Ndikumana ambaye alionekana kama beki bora wa Mbao Fc.
Ndikumana aliwaniwa na vilabu vitatu hivyo vyenye mashabiki wengi na ukwasi mkubwa wa noti, lakini mwishowe Ndikumana akasalia Mbao Fc hasa baada ya kuona anatakiwa kwa dau dogo wakati yeye ni staa wa Mbao Fc.
Kwasi alionekana si lolote si chochote ni mchezaji wa kawaida sana, hakutikisa kwenye vichwa vya habari vya magazeti yetu ya michezo hapa nchini, mzaliwa huyo wa Ghana aliyezaliwa miaka 25 iliyopita akaachwa aende zake, kijana wa watu akajiunga na Lipuli Fc ya Iringa timu iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.
Simba yenyewe iliishua kumuona Emmanuel Mseja, wakati Yanga Sc ikamuona Pius Buswita, na Azam Fc ikamnasa Salmin Hoza, na hao ndio wakaonekana wachezaji bora wa Mbao Fc mpaka kusajiliwa na klabu kubwa za hapa Tanzania, Asante Kwasi akiwa na Lipuli yake aliweza kuisaidia timu hiyo kupambana na hatimaye ikavivimbia vigogo Yanga na Simba.
Lipuli ilianza kuibana Yanga katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ikitoka nayo sare ya bao 1-1, Kwasi alionekana kuwa kikwazo kwa Yanga, hasa baada ya kumdhibiti vilivyo kiungo wa mabingwa hao watetezi, Mkongoman, Papy Kabamba Tshishimbi.
Kwasi pia akaishika na Simba baada ya Lipuli kutoka nayo sare ya 1-1 uwanja wa Uhuru pia, beko huyo aliisawazishia Lipuli kwa goli lake zuri la kichwa, kuanzia hapo Simba walianza kumvizia na kisha wakafanikiwa kumsajili moja kwa moja kwa ada ya shilingi Milioni 25 za Kitanzania.
Beki huyo anayesifika kwa upachikaji, hadi anahamia Msimbazi alikuwa amefunga magoli matano, na alipoanza kazi Simba akafanikiwa kufunga bao moja na sasa ana mabao sita akichuana vikali na washambuliaji Ibrahim Ajibu wa Yanga, Shiza Kichuya wa Simba, Marcel Boniventure wa Majimaji na Mohamed Rashid wa Tanzania Prisons wenye mabao sita kila mmoja.
Na kwa uchezaji wake kwa vyovyote anaweza kabisa kuipa taji la 19 Simba Sc msimu huu wa 2017/18, Simba imekosa ubingwa wa Bara zaidi ya misimu mitatu, Asante Kwasi pia amewahi kuichezea Mbabane Swallors ya Swaziland timu ambayo pia alikuwa akiichezea kiungo wa Yanga, Mkongoman Papy Kabamba Tshishimbi