OKWI AFICHUA KILICHOMRUDISHA VPL
Na Salum Fikiri Jr. Dar es Salaam
Mshambuliaji wa kimataifa wa Simba Sc, Emmanuel Okwi raia wa Uganda, hatimaye ameweka wazi kufeli kwake kucheza soka la kulipwa katika nchi za Tunisia na Denmark.
Kinara huyo wa magoli, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) amefichua kuwa, alishindwa kucheza nchini Tunisia na kuvunja mkataba na klabu ya Etoile du Sahel aliyojiunga nayo akitokea Simba Sc ya Tanzania ni kwa sababu timu hiyo ilishindwa kumlipa mshahara wake wa miezi mitatu.
Okwi amesema timu hiyo ilianguka kiuchumi na ikajikuta ikishindwa kuwalipa wachezaji wake wengi na wengine kutimka, pia akaelezea kushindwa kwake Denmark na kuvunja mkataba na klabu ya Sonderjyske baada ya timu hiyo kushindwa kumpa nafasi ya kucheza.
"Sikuwa chaguo la kwanza kwenye klabu hiyo hivyo nikapoteza nafasi kwenye timu ya taifa ya Uganda na sikuweza kuitwa tena kwenye timu hiyo hivyo nikakaa chini na viongozi pamoja na wakala wangu na kuamua kuvunja mkataba ili nikatafute nafasi kwingine", alisema Okwi ambaye akaamua kurejea Simba na sasa amekuwa msaada mkubwa katika klabu hiyo inayosaka taji la VPL kwa udi na uvumba