Kispoti

NAUONA MWISHO MBAYA WA TSHABALALA SIMBA.

Na Prince Hoza

HALI si shwari kwa maisha ya Mohamed Hussein "Tshabalala" au Zimbwe Jr ndani ya klabu ya Simba, na hii yote inatokana na usajili uliofanywa na klabu hiyo mwanzoni mwa msimu huu.

Simba imefanya usajili mkubwa wa kuongeza wachezaji wapya 13 ambao wameweza kuleta chachu kwenye kikosi hicho ambacho kwa sasa kinaongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 42 ikishuka dimbani mara 18 ikifuatiwa na mahasimu wao Yanga Sc wenye pointi 37 nao wamecheza mechi 18.

Azam Fc inakamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 35 yenyewe ikicheza mechi 19, Singida United inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 34 nayo ikicheza mechi 19.

Katika misimu miwili iliyopita, Mohamed Hussein "Tshabalala" alikuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Simba, Tshabalala pia ameweza kushinda tuzo mbalimbali za uchezaji bora za klabu na za Ligi Kuu ya Vodacom.

Lakini kubwa zaidi ni pale alipoweza kuzoa tuzo mbili kubwa, ya kwanza ni ile inayotolewa na klabu yake ya Simba, ambapo ilimtunuku tuzo ya mchezaji Bora wa mwaka na pia akashinda tuzo nyingine ya mchezaji bora wa mwaka wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Maisha ya Tshabalala ndani ya Simba yalikuwa supa, kinapofika kipindi cha usajili, jina lake linakonga kurasa za magazeti ya michezo, Tshabalala akitajwa kutua Yanga, na akiwa mtaani Tshabalala anakuwa mfalme, gari lake alilozawadiwa na mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe linasukumwa na mashabiki.

Ama kweli Tshabalala alijipatia heshima kubwa, Tshabalala si mkubwa wa umbo, ila ana jina kubwa hapa nchini, na aliweza kuwa mlinzi bora wa kushoto hapa nchini, Tshabalala hakuwa na mpinzani si kwenye timu ya taifa, Taifa Stars wala katika klabu yake ya Simba.

Makocha wote aliokutana nao iwe Simba au Stars hawakuwa na shaka nao, lakini sifa nyingi alizozipata zilitokana na bahati yake binafsi, kijana huyo aliweza kuwateka mashabiki wa Simba hasa kutokana na kasi yake uwanjani.

Kuna wakati Tshabalala akalikataa jina hilo alilopachikwa na mashabiki wa soka kutokana na uchezaji wake kufanana na ule wa mchezaji wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana, Siphiwe Tshabalala.

Kikosi cha kwanza cha Simba lazima Tshabalala awepo na alikuwa na kasi ya aina yake, beki huyo wa kupanda na kushuka alisajiliwa na Simba akitokea Kagera Sugar ya Bukoba.

Mabadiliko yaliyofanywa na Wekundu hao hasa mwanzoni mwa msimu huu wakisajili wachezaji wapya 13 wakiwa na malengo ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara unaoshikiliwa na mahasimu wao Yanga.

Tshabalala na kung' ara kote hakuwahi kubeba taji la VPL, Simba imeshapitiliza misimu minne sasa bila kutwaa kombe hilo, mara yao ya mwisho Simba kutwaa ubingwa wa bara ilikuwa msimu wa 2011/12 na baada ya hapo Yanga ikatwaa ubingwa huo huku ikipokezana kijiti cha uongozi na Azam Fc.

Simba yenyewe iliishia kuongoza ligi mzunguko wa kwanza tu, lakini mwishowe taji linaenda kwingine, Tshabalala licha ya uhodari wake lakini hakuweza kusaidia lolote ndani ya Simba kuhusu kupatikana ubingwa wa Bara, hakuwahi kufunga wala kutengeneza bao (Asist).

Msimu huu Wanasimba wamechoka, wanataka ubingwa wa bara kwa hali na mali, na kwa hesabu zao makocha, wameona Tshabalala hatoshi kusimama katika kikosi cha kwanza na kuipa taji Simba.

Simba ikaamua kuwaleta mabeki wengins wa pembeni ili kumpa changamoto Tshabalala, mabeki hao ni Jamal Mwambeleko, Erasto Nyoni na Mghana, Asante Kwasi, lakini Mwambeleko hakuweza kumng' oa Tshabalala katika kikoai cha kwanza, na Nyoni naye ni kiraka lakini Asante Kwasi akaitwaa namba ya Tshabalala, na sasa Tshabalala anatafutiwa nafasi nyingine ya kucheza au amsubiri Kwasi awe na kadi tatu za njano ndio acheze.

Kwasi anajua kufunga na tayari ameshafunga goli moja lililochangia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Singida United, lakini pia Kwasi ana mabao sita kwa ujumla, Kwasi alifunga mabao matano akiwa Lipuli, amepiga pasi nyingi za mwisho zilizozaa mabao ya Simba ikipata ushindi, Leo hii nauona mwisho mbaya wa Tshabalala Simba

Alamsiki

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA