Kispoti

Yanga na nyie jengeni utaratibu wa kuwatibia wachezaji wenu nje ya nchi.

Na Prince Hoza

YANGA SC juzi imepata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Saint Louis ya Shelisheli mchezo wa Raundi ya awali Ligi ya mabingwa barani Afrika katika uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Kwa maana hiyo Yanga inahitaji kujilinda zaidi ugenini zitakaporudiana ili isiruhusu kipigo cha mabao 2-0 kwani ikipata kipigo hicho itakuwa imeondoshwa mashindanoni, tatizo kubwa kwa upande wa Yanga lilionekana kwenye sehemu ya ufungaji.

Yanga ilishindwa kupenya ukuta wa Saint Louis, hadi mapumziko timu hizo zilienda zikiwa hazijafungana, Yanga iliongoza kwa kumiliki mpira ikishambulia mara kwa mara, mabeki wa Saint Louis walikuwa imara kuzuia hatari zote.

Wachezaji karibu wote wa Saint Louis walirudi nyuma kuzuia wasifungwe mabao mengi, kwa upande wa Yanga tatizo lilionekana kwenye sehemu ya ushambuliaji kwani hawakuwa na mtu mwenye uwezo wa kuingia na mpira katikati ya msitu wa mabeki wa Saint Louis.

Obrey Chirwa na Pius Buswita hawakuwa na mbinu mbadala za kupenya ukuta wa Louis, goli pekee walilolipata lilitokana na miujiza tu ya mpira wa kona ya Geofrey Mwashiuya iliyounganishwa na Juma Mahadhi dakika ya 66 ambao wote waliingia kwa pamoja.

Yanga inapitia msoto huu kwa sababu washambuliaji wake tegemeo Amissi Jocelyin Tambwe raia wa Burundi, Donald Ngoma raia wa Zimbabwe na Thabani Scara Kamusoko kuwa majeruhi, nyota hao wa kigeni ndio tegemeo kwa upachikaji wa mabao.

Ngoma akiwa kwenye ubora wake kabla hajakumbwa na majeraha alikuwa na uwezo mkubwa wa kuingia na mpira hata kukiwa na msitu wa mabeki, kukosekana kwake kumeweza kuiathili Yanga hasa kwenye eneo la ushambuliaji.

Mzimbabwe huyo alianza kuandamwa na majeraha tangu mwanzoni mwa msimu uliopita ambapo aliishia kucheza mzunguko wa kwanza na kumalizia msimu benchi, na msimu huu vilevile, Ngoma ameanza kucheza mzunguko wa kwanza na amecheza mechi chache.

Obrey Chirwa, Pius Buswita na Ibrahim Ajibu ndio wamekuwa tegemeo la Yanga kwenye safu ya ushambuliaji na wameshindwa kuwafurahisha mashabiki wa Yanga kama ilivyokuwa kwa Ngoma na Tambwe.

Tambwe naye anaandamwa na majeraha aliyoyapata kwenye kipindi cha maandalizi ya kuelekea msimu huu, na hadi sasa bado hajawa fiti kwa asilimia 100, kiungo mshambuliaji Mzimbabwe, Thabani Kamusoko ambaye aliiweka Yanga kwenye matawi ya juu, Kamusoko amepatwa na majeraha mwanzoni mwa msimu huu ambayo yanamtesa.

Jinsi majeruhi hao wanavyopatiwa matibabu yao hapa nchini hayaonyeshi dalili za kurejea uwanjani na ufiti wao wa awali, Yanga jumla ina majeruhi karibu 11 ambao wanaonekana kuigharimu timu hiyo, majeruhi hao ni Youthe Rostand, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Andrew Vincent "Dante", Pato Ngonyani, Yohana Nkomola, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Ibrahim Ajibu.

Pengo la Tambwe, Ngoma na Kamusoko bado linaonekana ingawa Papy Kabamba Tahishimbi amekuwa akiimudu, ila Tshishimbi aliletwa Yanga kwa ajili ya kuziba pengo la Frank Domayo aliyeihama Yanga na kutimkia Azam Fc miaka minne iliyopita.

Katika miaka minne pengo la Domayo lilionekana kuiathili Yanga na imewachukua muda kuziba mpaka Tshishimbi alipoletwa kuziba, lakini kitendo cha Tshishimbi kwenda kucheza namba ya Kamusoko eneo la namba sita linaonekana kuathilika.

Frank Domayo alikuwa majeruhi wa muda na klabu ya Azam ilipomsajili ikaamua kumpeleka nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na tiba, ikabainika kiungo huyo fundi alikuwa akicheza Yanga na majeraha yake.

Sijawahi kusikia hata mara moja uongozi wa Yanga ukizungumzia kuwapeleka wachezaji wake walio kwenye majeruhi nje ya nchi kwa matibabu, haya yote yanatokana na wao na ndio maana mashabiki wa Yanga wanakosa raha.

Leo hii kama Donald Ngona, Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko wangekuwa wameshapatiwa matibabu nje ya nchi, iwe India au Afrika Kusini huenda wangeisaidia timu yao kuiua Saint Louis, Simba wao wamekuwa na utaratibu mzuri wa kuwapeleka nje ya nchi wachezaji wake wenye majeraha hata Azam nao wana utaratibu wa kuwapeleka nje majeruhi wake.

Simba imempeleka nchini India, kipa wake wa pili, Said Mohamed Nduda, Yanga na nyie jengeni utaratibu wa kuwapeleka nje ya nchi wachezaji wenu wanaoandamwa na majeruhi hasa wale tegemeo ili wawasaidie kutetea taji la VPL na kufanya vema kimataifa, KWA LEO NAISHIA HAPA, TUKUTANE JUMA LIJALO

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA