KISPOTI
ALICHOFANYA JUMA NYOSO ANGEKUWA SIMBA SC INGEKUWA POA.
Na Prince Hoza
JUMATATU ya wiki iliyopita beki wa Kagera Sugar Juma Said Nyoso alimpiga shabiki wa Simba Sc mpaka kuzimia, Nyoso alifanya hivyo baada ya shabiki huyo kumpulizia vuvuzela masikioni mwake.
Tayari Nyoso alikuwa na hasira kufuatia timu yake ya Kagera Sugar kuchapwa mabao 2-0 na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Inasemekana shabiki huyo alianza kumuandamana Nyoso tangu dakika 90 za mchezo, na baada ya mpira kumalizika shabiki huyo aliingia uwanjani akiwa na vuvuzela lake na kumkaribia Nyoso kisha kumpulizia masikioni mwake kama sehemu ya kuwasilisha furaha yake.
Ikumbukwe msimu uliopita mashabiki wa Simba walitoka vichwa chini katika uwanja huo baada ya timu yao kulala kwa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, hivyo furaha ya kupitiliza waliyokuwa nayo wapenzi na mashabiki wa Simba ilizidi mipaka baada ya timu yao kulipiza kisasi na kumfanya shabiki huyo kumkera Nyoso.
Ni kweli kitendo alichokifanya shabiki huyo cha kushangilia timu yake si kibaya na wala si cha kukera, mashabiki wa vilabu vikubwa hapa nchini Simba na Yanga huwa wanapenda furaha muda wote.
Hawapendi kuhuzunika pale timu yao inapocheza, tumeshuhudia msimu uliopita mashabiki wa Simba walipong' oa viti vya uwanja wa Taifa Dar es Salaam wakipinga mwamuzi Martin Saanya kumtoa kwa kadi nyekundu mchezaji wao Jonas Mkude.
Hivyo kitendo cha shabiki huyo kushangilia sana timu si dhambi, lakini shabiki huyo alianza kumshambulia kwa matusi Juma Nyoso muda wote wa mchezo haukuwa uungwana na hasa beki huyo alipocheza vizuri kipindi cha kwanza.
Nyoso aliumudu vema mchezo huo akifanikiwa kuwadhibiti washambuliaji wa Simba wasilete madhara langoni kwa Kagera Sugar, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana, inasemekana shabiki huyo hakufurahishwa na uchezaji wa kibabe wa Juma Nyoso kwa washambuliaji wa Simba mpaka kushindwa kufunga katika ingww ya kwanza.
Lakini kipindi cha pili Simba ilikuja na kasi mpya na kufanikiwa kufunga mabao hayo mawili, kwa furaha ya shabiki huyo akaamua kumsogelea Nyoso na kumpulizia vuvuzela masikioni mwake.
Nyoso akiwa na hasira za kufungwa kisha kutukanwa na pia kupuliziwa vuvuzela masikioni na ikiwa yeye si mtu wa matani akaamua kumtwanga shabiki huyo mpaka kupelekea kuzimia, Nyoso naye akakamatwa na polisi kwa kitendo hicho.
Baada ya kukamatwa na polisi, mengi yamezungumzwa kuhusu Nyoso, kila mmoja amesema lake, wapo waliomshutumu Nyoso kwa shambulio hilo lakini pia wapo waliomsifu, ila waliomshutumu ni wengi kuliko waliomsifu.
Kwa bahati mbaya sana Nyoso anaichezea Kagera Sugar ya Misenyi, Bukoba mkoani Kagera, timu hiyo hain a mashabiki wengi kama ilivyo Simba Sc na ndio maana ilikuwa rahisi kumuandama Nyoso hadi kufikia hatua ya kumlaza rumande, sijawahi kusikia mchezaji wa Simba au Yanga akilazwa rumande kwa kupiga shabiki au kutukana.
Nahisi tukio lile angelifanya Nyoso wa Simba Sc sidhani kama angekamatwa ama kushutumiwa, mbona hawakukamatwa wale mashabiki wahuni waliong' oa viti uwanja wa Taifa msimu uliopita.
Kwa Nyoso wa Kagera Sugar imekuwa rahisi kuchukuliwa hatua kiasi kwamba hata Shirikisho la mpira wa miguu nchini, (TFF) nalo linajiandaa kumpa adhabu ya kumfungia mechi tatu na faini ya shilingi laki tano.
Lakini Nyoso huyu huyu aliwahi kumtomasa makalioni Amir Maftah wa Yanga, wakati huo Nyoso alikuwa anaichezea Simba Sc na hakuna mtu aliyetoa maoni, Maftah baada ya kufanyiwa udhalilishaji huo aliamua kurusha ngumi, refa alimuona na kumtoa kwa kadi nyekundu ambayo ilikuja kumgharimu na kuonekana msaliti kisha kutemwa na timu yake msimu uliofuata.
Katika mchezo huo wa watani, Simba iliifunga Yanga mabao 4-3 mchezo ukiwa wa Ligi Kuu Bara, Maftah alionekana msaliti kwa kufanya kosa la makusudi, lakini kiukweli alidhalilishwa na Nyoso.
Umefika wakati sasa kila mmoja amheahimu mwenzake, tuache ushabiki wa kishamba kwa kuingia uwanjani na kuwafanyia dhihaja wachezaji, leo hii Nyoso yuko Kagera Sugar kesho atakuwa Simba sijui utafanyaje hapo.
Ni kweli Nyoso amekosea kwa kujichukulia sheria mwenyewe lakini kosa hilo hilo angelifanya akiwa na Simba kwa vyovyote angesifiwa na kuungwa mkono, au shabiki yule wa Simba angempiga Nyoso ingekuwa poa tu
Tukutane Ijumaa ijayo kwenye makala yangu nyingine ya Staa wetu