KISPOTI
SIMBA SASA IMEAMUA KULETA KOCHA KIBURI NA JEURI ZAIDI YAO
Na Prince Hoza
NIMESOMA vizuri rekodi ya kocha mpya wa Simba Sc, Mfaransa Pierre Lechantre kuwa hakuwahi kudumu na timu zaidi ya mwaka mmoja, lakini klabu ya Simba nayo haijawahi kudumu na kocha kwa kipindi cha mwaka mmoja au zaidi.
Joseph Omog peke yake ndiye aliyedumu kwa mwaka mmoja na zaidi na ameweza kwa sababu aliiwezesha Simba kurejea kwenye michuano ya kimataifa baada ya kukosa kwa miaka minne, Simba ilianza timua timua ya makocha tangu msimu wa 2011/12.
Pamoja na uongozi wa Simba kutoweka bayana muda wa mkataba wa kocha wake mpya Pierre Lechantre wa kuitumikia klabu hiyo, takwimu zinaonyesha Mfaransa huyo hajawahi kukaa katika klabu moja zaidi ya mwaka.
Uongozi wa Simba umemtangaza Mfaransa Lechantre kuwa kocha wa klabu hiyo akichukua mikoba ya Mcameroon Joseph Omog aliyetimuliwa hivi karibuni, ujio wa kocha huyo Mfaransa unaifanya Simba kuwa imefundishwa na makocha tisa tangu ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2012/13 ikiwa chini ya Mserbia Milovan Cirkovic.
Kwa mujibu wa Mtandao wa http://www.transfermark.hezrog.kr.com unaojihusisha na kutoa takwimu za masuala mbalimbali ya michezo umeonyesha kocha Lechantre ana wastani wa kufundisha timu si chini ya mwaka kabla ya kuondoka ama kutimuliwa.
AVUNJA MKATABA SENEGAR
Mfaransa huyo aliwashangaza watu pale alipoamua kuvunja mkataba wake wa kuifundisha timu ya taifa ya Senegar wiki mbili baada ya kukubali kuchukua jukumu hilo mwaka 2012.
Lechantre aliiambia Senegar press Agency (APS) "Nilipata mkataba wiki iliyopita lakini hiyo siyo kigezo pekee cha mimi kuendelea na jukumu langu la kuiongoza timu ya Senegar kama wameshindwa kunitimizia matakwa yangu", alisema Lechantre.
Viongozi wa Senegar walishindwa kumlipa mshahara wake wa miezi sita aliyotaka alipwe kwanza kabla ya kuanza kazi, Mfaransa huyo.
LECHANTRE NA SOKA LA AFRIKA
Pierre Lechantre alianza kufundisha soka barani Afrika na timu ya taifa ya Cameroon, (Indonitable Lions) kuanzia Januari 1, 1999 hadi Juni 30, 2001 ni sawa na siku (911).
Baada ya hapo akatimkia Qatar akafundisha timu ya taifa ya nchi hiyo kuanzia Agosti 1, 2001 hadi Desemba 31, 2001 ni sawa na siku (152).
Akajiunga na klabu ya Al Ahli ya Qatar alidumu nayo kwa siku 123 ni kuanzia Julai 1, 2003 hadi Novemba 1, 2003 kabla ya kutimkia timu nyingine ya Al Sailiya pia ya Qatar aliyokaa kwa siku 242 kuanzia Novemba 1, 2003 hadi Juni 30, 2004.
Lechantre alirejea Afrika baada ya kupata mkataba wa kuifundisha Mali kwa muda mfupi kwa lengo la kuwapa tiketi ya kombe la dunia 2006, alifundisha hapo kwa siku 240 kuanzia Machi 5, 2005 hadi Oktoba 31, 2005.
Baada ya kushindwa kuipeleka Mali kombe la dunia 2006, Lechantre alitimkia katika klabu ya Al Rayyan ya Qatar akifundisha kwa siku 276, kuanzia Oktoba 1, 2006 hadi Juni 4, 2007, Kuanzia Julai 4, 2007 hadi Desemba 31, 2007 aliibukia Morocco na kujiunga na klabu ya MAS Fes aliyodumu nayo kwa siku 180 tu.
AWEKA REKODI YA KUDUMU NA KLABU MOJA TUNISIA.
Club Africain ya Tunisia ilimchukua Mfaransa huyo kuanzia Juni 12, 2009 hadi Aprili 8, 2010, na hiyo ndiyo klabu aliyokaa kwa muda mrefu zaidi, alidumu kwa siku 300, baada ya kuiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya pili ya kufuzu kwa Ligi ya mabingwa Afrika.
Mafanikio aliyoyapata Club Africain yaliwavutia miamba mingine ya Tunisia CS Sfaxien aliyokaa kwa siku 166 kuanzia Juni 22, 2010 hadi Desemba 5, 2010 kabla ya kutupiwa virago, Baada ya kuchemsha Tunisia, akatimkia Qatar na kujiunga na klabu ya Al Gharafa aliyokaa nayo kwa siku 196, kuanzia Machi 19, 2012 hadi Oktoba 1, 2012.
AWEKA REKODI YA KUDUMU NA TIMU SIKU 39 QATAR.
Kocha Lechantre aliweka rekodi ya kufundisha siku 39 katika klabu ya Al Arabi ya Qatar kuanzia Machi 19, 2012 hadi Aprili 27, 2012, baada ya kuondoka Qatar aliibukia Libya na kujiunga na klabu ya Al Ittihad aliyokaa kwa siku 187 kuanzia Machi 30, 2015 hadi Oktoba 3, 2015.
MWISHO MBAYA WA LECHANTRE CONGO BRAZAVILLE KABLA YA KUTUA SIMBA.
Kocha huyo mwenye bahati ya kufundisha mataifa ya Afrika alipata ulaji Januari 13, 2016 wa kuifundisha Congo Brazaville, lakini mkataba ulivunjwa ikiwa bado una miezi 17 mbele Novemba 5, 2016, Cingo Brazaville ilitangaza mkataba wake na kocha Lechantre baada ya kufungwa na Uganda bao 1-0 na kushindwa kufuzu fainali za kombe la dunia 2018.
Ni kama mkataba wa Simba na kocha huyo utakuwa kipimo kwa pande zote mbili, katika miaka minane Simba imefundishwa na Mfaransa Patrick Liewig, mzalendo Abdallah Kibaden, Mcroatia, Zdravko Logarusic, Mzambia, Patrick Phiri, Mserbia, Goran Kopunovic, Mwingereza, Dylan Kerr, Mganda, Jackson Mayanja na Mcameroon, Joseph Omog.
Mashabiki, wanachama na wapenzi wa Simba duniani kote wakiamini wamepata bonge la kocha, lakini watambue kocha mwenyewe si mkaaji sana kwenye klabu moja na hajawahi kudumu na timu mwaka mmoja na ndio mkataba wake na Simba umefanywa kuwa siri
KWA LEO NIMEISHIA HAPO, TUKUTANE TENA JUMA LIJALO