Yanga chali tena kwa Mbao
Na Paskal Beatus. Mwanza
Mabingwa wa soka Tanzania bara Yanga Sc jioni ya leo imeendelea kuwa mteja kwa vijana wa Mbao Fc baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Vijana wa Mbao wakicheza kandanda safi na kulisakama lango la Yanga lakini hadi mapumziko timu zote hazikufungana hata bao, kipindi cha pili Mbao Fc waliliandama lango la Yanga kama nyuki na kuandika goli la kwanza lililofungwa na Habibu Haji Kiyombo kunako dakika ya 53 kabla ya dakika ya 68 kuongeza bao la pili.
Kwa kipigo hicho Yanga wanashuka hadi nafasi ya nne ikiipisha Singida United ambayo jioni ya leo imeichapa Njombe Mji mabao 3-0 uwanja wa Sabasaba mjini Njombe, Singida imefikisha pointi 24 huku Yanga ikibaki na pointi 21 na kesho inaanza safari ya kuelekea visiwani Zanzibar kushiriki Mapinduzi Cup