STAA WETU

Simon Msuva: Mtanzania mwenye njaa ya mafanikio.

Na Prince Hoza

JICHO la kila Mtanzania lilikuwa kwa Mbwana Ally Samata anayeichezea timu ya Ligi Kuu Ubelgiji ya KRC Genk, Samata ni Mtanzania na mzaliwa wa Mbagala jijini Dar es Salaam ambaye amecheza Kimbangulile Academy, Mbagala Market (African Lyon), Simba SC na TP Mazembe ya DR Congo.

Samata amepata heshima kubwa kwenye mchezo wa soka na kuiweka pazuri Tanzania akisaidia kuitangaza, Samata amekuwa balozi mzuri akiwa na TP Mazembe ambapo amefanikiwa kubeba taji la Afrika na kuweza kushinda tuzo ya mwanasoka bora Afrika kwa mchezaji anayecheza ligi ya nyumbani, hakuna Mtanzania mwingine aliyewahi kushinda tuzo hiyo.

Baada ya mafanikio hayo, timu za Ulaya zikaanza kumtolea macho, na kwa bahati nzuri KRC Genk ikafanikiwa kumchukua na sasa ni mchezaji wa timu hiyo, tayari nyota yake inang' ara, akiisaidia timu hiyo kufanya vizuri kwenye Ligi ya Ubelgiji, na ubora wake ukapelekea kukamiwa mno na mabeki wa timu pinzani.

Na sasa Samata ni majeruhi baada ya kuumizwa wakati akiitumikia timu yake hiyo, baada ya Samata kuwa Mtanzania pekee anayefanya vizuri kwenye soka la kulipwa hasa kwa wachezaji wanaotokea Tanzania, jina lingine limechomoza na kumulikwa na wengi.

Si mwingine ni Simon Happygod Msuva na sasa macho yote ya Watanzania yameelekezwa kwake kwa sababu anafanya vizuri kwenye timu yake ya Difaa Hasaan El Jadida ya yenye maskani yake katika mji wa Casablanca, Morocco, timu hiyo inamilikiwa na bilionea wa Kiarabu, Sheikh Difaa Hassan Jadida anayemiliki visima vya mafuta.

Difaa El Jadida inashiriki Ligi Kuu ya Morocco inayojulikana kwa jina la Botola, Msuva amekuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo na mpaka sasa anachuana vikali kuwania ufungaji bora kwenye ligi hiyo.

Msuva ni kiungo mshambuliaji na karibu kila mechi amekuwa akiifungia timu hiyo mabao pamoja na kutoa pasi za mwisho (Assist), pia ni tegemep kwenye timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, umuhimu wake umeanza kuonekana katika siku za hivi karibuni hasa pale alipoweza kuifungia magoli dhidi ya Malawi na Burundi katika mechi za kirafiki.

Msuva alipata nafasi ya kujiunga na Difaa El Jadida ya Morocco baada ya kung' ara katika mashindano ya mataifa Afrika kwa nchi za ukanda wa kusini, (COSAFA CASTLE CUP) yaliyofanyika nchini Afrika Kusini Julai mwaka huu.

Msuva alikuwa miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars ambayo ilishiriki kama timu mwalikwa na kwa bahati nzuri ilitinga hatua ya nusu fainali na hapo ndipo Msuva alipopata zari la mentali la kwenda Morocco kujiunga na timu hiyo kubwa ya Casablanca, maisha ya Morocco ni kama ya Ulaya, Morocco ni nchi ya bara la Afrika lakini ipo Ulaya, kwa maana inapakana na mataifa ya Ulaya.

Kuna wakati taifa hilo lilitaka kujitoa katika Umoja wa Afrika na kujiunga na nchi za Ulaya, wenyewe wanaamini wapo Ulaya na ndio maana timu za Hispania, zimafuatilia ligi ya Morocco kwakuwa zimepakana, na hiyo itakuwa rahisi kwa Msuva kucheza Ulaya hasa Hispania na inasemekana timu ya Malaga inayoshiriki Laliga inamfuatilia Msuva na huenda ikamchukua mwakani.

Hivyo Watanzania wenzangu mnaodhani Msuva anacheza hapa hapa Afrika na hawezi kufika Ulaya, msijidanganye, Msuva miguu yake ipo Afrika lakini kiwiliwili chake kipo Ulaya, anacheza sehemu sahihi kabisa na kubwa, soka la Afrika ya kaskazini ni la daraja lingine tofauti na la Afrika mashariki, hata wawakilishi wa Afrika kwenye kombe la Dunia, Urusi mwakani, nchi za kaskazini zimetoa wawakilishi watatu kati ya watano kutoka Afrika, Morocco ikiwemo.

Ninaamini Msuva anaweza kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika ligi kubwa barani Ulaya, Morocco ni njia ya kumfikisha huko kwani wachezaji wengi duniani wamepitia hapo.

Mchezaji huyo amezaliwa Desemba 3, 1993 jijini Dar es Salaam, na alianza kucheza soka tangu utotoni, aliibukia timu za mchangani akianzia mtaani kwao Kimara kabla ya mwaka 2010 kujiunga na Azam FC hadi 2011, inasemekana Msuva aliwahi kupelekwa Simba B na baba yake mzazi mzee Happygod lakini viongozi wa Simba walimkataa nsipo alipopelekwa Azam FC akianzia Academiya.

Maisha yake ndani ya Azam FC hayakuwa mazuri kwani alikuwa miongoni mwa wachezaji walioachwa, mwaka 2011 aijiunga na Moro United iliyokuwa na makazi yake Dar es Salaam, hapo ndipo Msuva alipoonyesha kipaji chake  na kunyakuliwa na Yanga SC kuanzia mwaka 2012 alipodumu hadi mwaka huu 2017  alipojiunga na Difaa El Jadida ya Morocco.

Msuva ana njaa ya mafanikio na hiyo ndiyo silaha yake inayomfanya ang' are uwanjani, mchezaji huyo amekuwa akijituma mno na kumfanya akubalike mashabiki wa timu yake kuanzia Yanga na sasa Difaa, Msuva ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu bara akiwa na Yanga, kombe la FA, na Klabu bingwa Afrika mashariki na kati mara mbili yote akiwa na Yanga, kwahiyo hakuna cha kupoteza kwake, huku pia akifanikiwa kushinda tuzo za ufungaji bora.

Mshambuliaji huyo aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2014/15 akifunga magoli 17 na msimu uliopita wa 2016/17 aliibuka tena mfungaji bora akifunga magoli 14, Msuva pia ana rekodi ya kuifunga Simba mara mbili kwa nyakati tofauti,  zote akiwa na Yanga.

Mbali na kushinda tuzo hizo mbili za ufungaji bora VPL, Msuva amewahi kushinda pia tuzo ya ufungaji bora wa kombe la Mapinduzi mwaka 2015 akifunga magoli manne, nyota yake imeendelea kung' ara kiasi kwamba alienda kufanya majaribio katika timu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

Kwa bahati mbaya dili la kujiunga na timu hiyo lilishindikana, lakini Mungu si Athuman mwaka huu 2017, Msuva akachukuliwa moja kwa moja bila kufanya majaribio na Difaa El Jadida ambapo pia klabu yake ya Yanga iliridhia pasipo kumwekea kauzibe

TUKUTANE TENA JUMATATU IJAYO KATIKA UCHAMBUZI WA KISPOTI

Simon Msuva 

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA