Nitafanya mambo makubwa Ndanda- Ngasa
Na Mwandishi Wetu. Mtwara
Mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngasa amesema atafanya mambo makubwa akiwa na kikosi chake kipya cha Ndanda FC ya mkoani Mtwara alichojiunga nacho katika usajili wa dirisha dogo la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Ndanda inakutana na Simba Jumamosi ijayo katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mchezo wa Ligi Kuu bara na Mrisho Ngasa amesema mchezo huo utakuwa muhimu kwake kwani wapenzi na mashabiki wa Ndanda wanampa matumaini makubwa ya kufanya vizuri akiwa na kikosi hicho.
Ngasa amefunguka kuwa anajisikia furaha kucheza Ndanda na hata kiwango chake anaamini kinaweza kurejea kama zamani, amewataka Wanamtwara kujitokeza kwa wingi na kuiunga mkono timu yao ya nyumbani itakavyotoa ushindani kwa Simba iliyojeruhiwa.
Simba ilitolewa katika michuano ya FA baada ya kufungwa mabao 4-3 kwa mikwaju ya penalti kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Green Warriors ya daraja la pili, matokeo yaliyosababisha kufukuzwa kazi kwa kocha wao mkuu, Mcameroon, Joseph Marius Omog.