KISPOTI

Simba walikuwa bize na Asante Kwasi wakawasahau Shaaban Dihile na Hussein Bunu.

Na Prince Hoza

KIUNGO Jonas Gerald Mkude aligongesha mwamba penalti yake na Mohamed Hussein "Tshabalala" akamdakisha kipa wa zamani wa kimataifa nchini Shaaban Dihile, Simba ikitolewa hatua ya 64 bora, sawa na raundi ya pili tu ya kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) maarufu kombe la FA, Ijumaa iliyopita.

Maana yake Simba SC imevuliwa ubingwa wa Azam Sports Federation Cup, baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na timu ya Green Warriors ya Mwenge Dar es Salaam inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania, (JWTZ).

Katika mchezo huo uliofanyika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kipa wa Simba Aishi Manula alipangua penalti moja ya Zuakuu Mgala kabla ya George Ossey kupiga nje, lakini penalti za Cecil Efraim, Amir Haji, Juma Mdingi na Iddi Nyambi zilimpita.

Katika dakika ya 90 za mchezo huo, Green Warriors walitangulia kupata bao dakika ya 43 kupitia kwa mshambuliaji Hussein Bunu aliyefunga kwa kichwa akimalizia kazi nzuri ya Gido Chawala.

Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha pili, ambako Simba walifanikiwa kusawazisha dakika ya 53 kwa penalti ya kiufundi ya nahodha John Raphael Bocco "Adebayor" baada ya Amir Haji kuunawa mpira kwenye boksi katika harakati za kuokoa.

Kutoka hapo, Simba walifunguka zaidi na kuanza kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Green Warriors lakini sifa za kipekee zimuendee kipa wa kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki fainali za CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast, Shaaban Dihile aliyeokoa michomo mingi ya hatari.

Mwishoni mwa mchezo, refa mkongwe Israel Nkongo alimuonyesha kadi ya njano Adam Said wa GreenbWarriors na kumtoa kwa kadi nyekundu hivyo wakacheza pungufu dhidi ya mabingwa watetezi Simba.

Makocha wote wa Simba Mcameroon, Joseph Marius Omog, wasaidizi wake, Mrundi Masoud Djuma na mzalendo Muharammi Mohamed "Shilton" ambaye ni kocha wa makipa walijadiliana vizuri wakati wa kuchagua wapiga penalti.

Kocha wa Green Warriors, Azishi Kondo alikuwa mwenye furaha baada ya mechi kwa kuwatoa Simba ambao ni mabingwa watetezi pia ndio vinara wa Ligi Kuu bara, bali pia ni timu yenye makocha wawili wa kigeni na wachezaji nyota na ghali huku pia ikitajwa kuwa ndio timu tajiri zaidi kwa sasa baada ya uwekezaji mkubwa wa kikosi chake cha shilingi Bilioni 1.3 za Kitanzania.

Lakini kama walivyosema wahenga "Siku ya kufa nyani miti yote huteleza" pamoja na Aishi Manula kuokoa penalti moja ya GreennWarriors lakini haikuisaidia Simba kusonga mbele na ikatolewa mapema zaidi tena na timu ya Daraja la kwanza.

Ukikitazama kikoai cha Green Warriors cha kipa Shaaban Dihile, Edward William, Amir Haji, Cecill Efraim,  George Osey, Iddi Nyambi, Gido Chawala, Thomas Ndimbo, Adam Said, Mohamed Athuman, Hussein Bunu, Juma Mdingi na Hassan Gumbo.

Wakati Simba ya bilioni 1.3 ikiwa kamili na kipa wake Tanzania One, Aishi Manula, Erasto Nyoni, Ally Shomari, Mohamed Hussein "Tshabalala", Yusuph Mlipili, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, John Raohael Bocco, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto na Moses Kitandu.

Katika kikosi cha Green Warriors wazoefu wa soka la Tanzania ni Shaaban Dihile, George Ossey na Hussein Bunu, na Simba waliwasahau nyota hao waliowahi kuichezea JKT Ruvu iliyokuwq kwenye ubora wake, JKT Ruvu ilikuwa ikiisumbua sana Simba na kuifunga mara moja moja, Hussein Bunu amewahi kuifunga Simba mara kadhaa, alikuwa mmoja kati ya vinara wa mabao Ligi Kuu bara.

Lakini Simba waliwasahau kabisa watu hao, walijua wanakutana na kitimu cha daraja la pili hivyo kufungwa haiwezekani, kuna mazoea kwamba timu kubwa kama Simba au Yanga haifungwi na timu ndogo hasa za daraja la pili na ikitokea imefungwa basi kocha anafukuzwa na ndivyo ilivyotokea kwa Mcameroon, Joseph Marius Omog alivyofutwa kazi.

Viongozi wa Simba wao walikuwa bize na Asante Kwasi, hata mashabiki wake nao furaha yao ilikuwa kumpata Kwasi, ambaye aliwahi kuwasurubu wakati Lipuli FC ya Iringa ikienda sare ya 1-1 na Simba, uwanja wa Uhuru Dar es Salaam mchezo wa Ligi Kuu bara.

Asante Kwasi raia wa Ghana alisajiliwa kimakosa na Simba hivyo kuzua mjadala mzito uliofikia muafaka baada ya uongozi wa Simba kuiandikia barua Lipuli ili ipewe ridhaa ya kumsajili Kwasi, na uongozi wa Lipuli uliridhia Kwasi ajiunge na Simba.

Furaha ya Simba kumpata Kwasi walisahau kila kitu, walisahau kama wana mchezo wao wa kombe la Azam Sports Federation Cup dhidi ya timu ya daraja la pili ya Green Warriors inayomilikiwa na wanajeshi.

Walisahau kama timu hiyo ina nyota Shaaban Dihile "Tanzania One" wa kitambo na straika matata Hussein Bunu mfungaji bora wa miaka hiyo, wanewasahau kabisa watu hao na ndio maana ikawa rahisi Bunu kumfunga kwa kichwa Tanzania One wa sasa Aishi Manula, ndio maana ikawa rahisi Shaaban Dihile kudaka penalti ya Tshabalala na vijana wa Green Warriors kutinga hatua ya 32 bora

NAWATAKIA SIKUKUU NJEMA YA CHRISTMASS NA MWAKA MPYA

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA