DK SHEIN AWAJAZA MAMILIONI WACHEZAJI, ZANZIBAR
Na Mwandishi Wetu. Zanzibar
Rais wa serikali ya Baraza la mapinduzi, Zanzibar, Dk Mohames Ally Shein, jana amewazawadia wachezaji wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, makocha wake pamoja na viongozi kila mmoja shilingi Milioni 3 za Kitanzania na kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, baada ya kuiwezesha Zanzibar kushika nafasi ya pili kombe la Chalenji.
Rais Shein amewatunuku mashujaa hao licha ya kufungwa kwa penalti na wenyeji Kenya katika mchezo wa fainali ulioisha kwa sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 120 katika uwanja wa Kemyatta, mjini Machakos nchini Kenya.
Zanzibar ilipangwa kundi A pamoja na timu za taifa za Rwanda, Libya, Tanzania bara na Kenya na kuweza kukamata nafasi ya pili ikiwa nyuma ya wenyeji Kenya waliomaliza vinara, katika mchezo wa nusu fainali, Zanzibar iliiondosha Uganda ambao walikuwa mabingwa watetezi.
Tangia mwanzo Zanzibar ilionekana kuhimili mikiki mikiki ya michuano ambapo katika mchezo wake wa kwanza iliweza kuilaza Rwanda mabao 3-1 kabla ya kuilaza Tanzania bara 2-1 na kisha kutoka sare tasa 0-0 na Kenya kabla ya kulala 1-0 kwa Libya.