AZAM FC KUISHUSHA KILELENI SIMBA LEO?
Mrisho Hassan. Dar es Salaam
Klabu bingwa Afrika mashariki na kati, Azam FC usiku wa leo inaikaribisha Stand United katika uwanja wake wa Azam Complex uliopo Chamazi mjini Dar es Salaam, mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Endapo Azam FC itaibuka na ushindi wa aina yoyote dhidi ya wapiga debe hao wa Stand, basi itakuwa imeishusha kileleni Simba na kuongoza ligi hiyo, Azam ina pointi 23 sawa na Simba ila imezidiwa magoli ya kufunga.
Mechi nyingine za ligi hiyo zitapigwa kesho hadi keshokutwa, kesho Desemba 30 mwaka 2017 Lipuli itaialika Tanzania Prisons uwanja wa Samora mjini Iringa wakati Mtibwa Sugar ikiwakaribisha Majimaji uwanja wa Manungu Complex.
Ndanda FC nao watawakaribisha Simba SC uwanja wa Namgwanda Sijaona mjini Mtwara wakati siku ya Jumapili Desemba 31, 2017 Njombe Mji itakuwa mwenyeji wa Singida United, Sabasaba Stadium mjini Njombe Mbao FC nao itakuwa mwenyeji wa Yanga SC, CCM Kirumba Mwanza, Januari 1, 2018 Mbeya City itaikaribisha Kagera Sugar uwanja wa Sokoine Mbeya na Mwadui itaawalika Ruvu Shooting uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga