Yanga yakwama kwa Prisons, Simba washindwe wenyewe
Na Mrisho Hassan. Dar es Salaam
Licha ya kucheza pungufu, vijana wa Tanzania Prisons jioni ya leo wamefanikiwa kuwabana mbavu wakongwe Yanga SC na kutoka nao sare ya kufungana bao 1-1 katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dares Salaam, mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Endapo Yanga ingeibuka na ushindi leo ingefanikiwa kukamata kiti cha usukani wa ligi kwani ingefikisha pointi 23 ikiziacha nyuma Simba na Azam zenye pointi 22 kila moja, hata hivyo sare hiyo imewapa pointi moja sasa wamefikisha pointi 21 wakiendelea kukaa katika nafasi yao ya tatu.
Prisons walikuwa wa kwanza kupata bao la uongozi likifungwa kipindi cha kwanza dakika ya 10 na mshambuliaji wake Eliud Mpepo lakini Yanga wakachomoa kupitia Raphale Daudi.
Prisons walionekana kuelemewa zaidi na kupelekea wachezaji wake kujiangusha hovyo na kupoteza muda, Ligi hiyo iliendelea katika viwanja vingine tofauti ambapo Ruvu Shooting ilishinda 2-1 dhidi ya Majimaji ya Songea uwanja wa Mabatini Mlandizi.
Hata hivyo mwamuzi wa mchezo huo aliwanyima Yanga bao la wazi kabisa lililofungwa na Obrey Chirwa aliyemalizia mpira uliotemwa na kipa wa Prisons, lakini mwamuzi alikataa akidai mfungaji ameotea.
Kagera Sugar na Stand United zilitoka sare 0-0 uwanja wa Kaitaba, Bukoba wakati Mbao FC ikiifunga Mwadui FC 1-0, CCM Kirumba Mwanza, ligi itaendelea kesho kwa mechi moja Simba SC na Lipuli uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam