Staa Wetu:
MRISHO KHALFAN NGASA. ANAPOTEA AU ANARUDI?
Na Prince Hoza
NIMEMUONA kwenye mechi zote mbili ambazo timu yake ya Mbeya City ilipocheza na miamba Simba na Yanga, mechi ambazo zilifuatana, ama kweli Mrisho Ngasa alicheza vizuri ingawa kikosi chake kilipoteza michezo yote hiyo.
Mbeya City ikicheza uwanja wa nyumbani wa Sokoine dhidi ya Simba SC iliyosheheni kikosi cha Shilingi Bilioni 1.3 za Kitanzania na kuonyesha ushindani mkubwa lakini Shiza Kichuya aliweza kuwalaza kwa goli lake la utatanishi ambalo inadaiwa lilikuwa la kuotea, katika mchezo huo Simba ilishinda bao 1-0.
Vijana hao wa Mbeya City walisafiri hadi Dar es Salaam kuwafuata mabingwa watetezi wa Ligi Kuu bara, Yanga SC mchezo uliofanyika uwanja wa Uhuru, Mbeya City ilifungwa mabao 5-0 ambayo yamezua mshangao mkubwa kwa mashabiki wa soka, wengi hawakuamini kipigo hicho hasa kwakuwa wanaifahamu fika Mbeya City.
Mbeya City ni moja kati ya timu zilizokuwa zikionyesha ushindani mkubwa hasa zinapokutana na Simba na Yanga, si rahisi rahisi timu hizo za Kariakoo kuondoka na pointi tatu.
Lakini ilikuwa kazi nyepesi vijana wa Jangwani kuvuna kalamu ya mabao, ikumbukwe katika kikosi cha Mbeya City kuna staa mmoja ambaye ni mkubwa sana, na staa huyo ana rekodi zake kwa hapa nchini sidhani kama kuna aliyezifikia ama kuzivunja.
Staa huyo si mwingine ni Mrisho Khalfan Chogi Ngasa, ambaye baba yake mzazi amewahi kuzichezea Pamba FC ya Mwanza, Simba SC ya Dar es Salaam na timu ya taifa, Taifa Stars na ile ya Tanzania bara, anaitwa Khalfan Chogi Ngasa ambaye aling' ara kama kiungo mshambuliaji na jina lake lilikuwa kubwa sana katika miaka ya tisini.
Mtoto wake ambaye ndio huyu Mrisho Ngasa amekuja kuwa staa mkubwa kuliko ilivyokuwa kwa baba yake, Ngasa ni Staa kwa sababu ana rekodi ya kuzichezea klabu zote tatu za Dar es Salaam yaani Yanga SC, Simba SC na Azam FC kwa mafanikio, pia ana rekodi ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi ya mabingwa barani Afrika.
Ngasa alikuwa mfungaji bora mwaka 2015 alipokuwa na klabu ya Yanga iliyotolewa kwenye raundi ya pili, Ngasa pia amewahi kuwa mfungaji bora katika michuano ya Chalenji miaka mitatu iliyopita ilipofanyika nchini Kenya, pia amewahi kuwa mfungaji katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Kiungi mshambuliaji huyo anajivunia mafanikio yake alipokuwa anaichezea Yanga SC ambapo alitamba nayo vilivyo na kuipa mataji, mwaka 2010 Ngasa alivunja rekodi ambayo mpaka sasa haijafikiwa hasa pale alipouzwa na Yanga kwa klabu ya Azam FC kwa dau nono la Shilingi Milioni 40 za Kitanzania.
Mpaka sasa hakuna klabu iliyomuuza mchezaji wake kwa klabu nyingine, Ngasa pia anajivunia kuwa Mtanzania wa kwanza kwenda kujaribiwa katika klabu ya West Ham ya Uingereza, Ngasa alipelekwa huko na wakala wake Yusuf Bakhresa.
Ambapo hata hivyo hakufaulu, pia aliwahi kujaribiwa nchini Marekani na timu ya Seatle Sounders inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani, katika majaribio hayo, Ngasa alicheza mchezo maalum wa kirafiki dhidi ya Manchester United iliyokwenda Marekani kufanya ziara, Mtanzania huyo aliweza kujitangaza duniani kutokana na ukubwa ilionao Manchester United.
Ili kudhihirisha Ngasa ni staa kama ilivyo kwa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu au Simon Msuva, ambao wanacheza soka la kulipwa ughaibuni, naye aliwahi kutakiwa na klabu ya Lov Ham ya Urusi lakini klabu yake ya Yanga ilinzuia, timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Urusi ilitaka kumsajili moja kwa moja bila kumfanyia majaribio.
Ngasa alijiunga na Azam FC ambapo pia alichez vizuri na kuwemo katika kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013/14, mchezaji huyo aliingia matatizoni na klabu yake hiyo na ikampeleka kwa mkopo Simba SC ambapo pia alicheza vizuri ingawa alidumu msimu mmoja na kurejea Yanga.
Ngasa hakudumu sana Yanga kwani alielekea nchini Afrika Kusini na kujiunga na klabu ya Ligi Kuu ya Free State Stars iliyokuwa ikinolewa na Mmalawi Kinnah Phiri ambaye baadaye alifundisha Mbeya City na kumvuta Ngasa, Nyota huyo alisaini mkataba wa miaka mitano lakini akavunja mkataba na kuelekea Oman kujiunga na timu ya Fanja FC, nayo hakudumu akarejea Tanzania alikojiunga na Mbeya City anayoichezea hadi sasa.
Ngasa aliyezaliwa Mei 5, mwaka 1989 jijini Dar es Salaam ni mwenyeji wa mikoa ya Mwanza anakotoka baba yake na Kagera anakotoka mama yake na kwa bahati nzuri mikoa yote hiyo walikotoka wazazi wake ameweza kuzichezea timu kubwa.
Safari yake ya soka ilianzia mwaka 2004 alipokuwa na kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Serengeti Boys ambapo aling' ara na kusajiliwa na Toto Africans ya Mwanza mwaka 2004, msimu uliofuata akajiunga na Kagera Sugar ambako pia aling' ara na kuchukuliwa na Yanga SC msimu uliofuatia.
JE! NGASA ANAPOTEA AU ANARUDI? NI JAMBO LA KUSUBIRI KISHA TUONE