Singida United yaibamiza Lipuli na kupaa
Na Mwandishi Wetu. Singida
Timu ya Singida United jioni ya leo imeutumia vema uwanja wake wa nyumbani wa Namfua baada ya kuilaza Lipuli ya Iringa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara raundi ya 10.
Bao pekee lililoipa pointi tatu Singida United lilifungwa na mshambuliaji wake Danny Usengimana raia wa Rwanda aliyepokea pasi toka kwa Salum Chuku, kwa ushindi huo Singida United inafikisha pointi 17 na ikikamata nafasi ya tano hivyo inakuwa imeishusha Tanzania Prisons ambayo kesho itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Simba.
Ligi hiyo inayoongozwa na Simba SC yenye pointi 19 itaendelea tena kesho kwa mechi nne kupigwa kwenye viwanja tofauti, Stand United itaialika Mwadui FC katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga, wakati Majimaji itakuwa mwenyeji wa Mbao FC katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Pale katika uwanja wa Sokoine Mbeya, Simba itakuwa mgeni wa Prisons na uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani, Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC ya Mtwara