KISPOTI

NENO LA HANSPOPPE KWA KAPOMBE, NDIO MANENO YA VIONGOZI WETU.

Na Prince Hoza

HIVI karibuni mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe aliibuka kwenye vyombo vya habari na kusema mchezaji wao Shomari Kapombe achague moja kati ya kucheza au kuondoka.

Hanspoppe amedai klabu ya Simba imechoka kumlipa mshahara mchezaji asiyecheza hivyo njia nzuri iliyomchagulia ni moja tu, kucheza au kuondoka, kiongozi huyo aliendelea kusema akidai Kapombe ameshapona majeraha yake yaliyokuwa yakimsumbua.

Kapombe alikuwa majeruhi  na tayari alishapona hivyo anatakiwa aanze kucheza, Hanspoppe alitanabaisha kuwa daktari wa klabu ya Simba, Yassin Gembe alianika ukweli kuwa Kapombe amepona ila hataki kucheza, Simba ilimsajili Kapombe mwanzoni mwa msimu huu akitokea Azam FC ambapo mkataba ulimalizika, na alisaini Simba kwa miaka miwili.

Moja kati ya usajili uiofurahiwa na Wanasimba wengi ambao waliamini ujio wake ungeleta faraja, Simba iliamua kumtema Mkongoman, Janviel Besala Bokungu ili kumpisha Kapombe ambaye anasifika kwa kupandisha mashambulizi mbele pia ni mmoja kati ya mabeki wanaofunga.

Kauli hiyo ya Hanspoppe iliwashangaza wengi hasa wapenda michezo wengi waliamini kauli ya Hanspoppe na kuona huenda Kapombe anafanya mzaha, lakini baadaye Shomari Kapombe akaibuka na kumjibu bosi wake akidai yeye bado hajapona na majeraha yake na anachosema Hanspoppe si kweli.

Kapombe amedai hawezi kucheza akiwa mgonjwa kwani anaweza kuhatarisha maisha yake ya kisoka, hivyo amemtaka Hanspoppe aache kuzungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu yeye kwani hawakuwahi kuzungumza wao wawili, Kapombe amesema kama Simba inataka kuvunja mkataba wake wavunje tu ili mradi wamlipe chake lakini hawezi kucheza akiwa hajapona.

Tangu asajiliwe mwanzoni mwa msimu huu, Kapombe hajacheza mechi yoyote si ya Ligi Kuu Bara ambayo kwa sasa imefikia raundi ya 11 wala mechi ya kirafiki.

Lakini hatujamsikia daktari wa klabu ya Simba, Yassin Gembe akielezea kupona kwa Kapombe na lini atarejea uwanjani, pia hatujamsikia kocha mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog akielezea kupona kwa Kapombe.

Maana hao ndio wanaohusika na masuala yote ya mchezaji hasa aliyeumia ambapo daktari wa timu ndiye msemaji mkuu, hata Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara hatujamsikia akielezea kupona kwa Kapombe.

Ina maana anachosema Hanspoppe hakina ukweli wowote, Hanspoppe amezitoa wapi taarifa za kupona Kapombe, kwani hakuwahi kuzungumza na Kapombe ambaye ndiye mhusika.

Tunafahamu fika kuwa Simba imemsajili Kapombe akiwa majeruhi, hata mimi nilishituka na kuwahi kutoa dukuduku langu juu ya usajili huo wa Kapombe ambaye aliandamwa na majeruhi ya mara kwa mara akiwa Azam FC.

Alipokuwa Azam FC, Kapombe aliwahi kuumia na kukosekana uwanjani kwa muda mrefu kama ilivyo sasa, lakini Azam FC walimpeleka nchini Afrika Kusini kumtibia na baadaye alirejea uwanjani, lakini tatizo kwake lilikuwa hilo hilo la kutonesha jeraha lake.

Kuna wakati Kapombe alikuwa kwenye timu ya taifa lakini majeraha yake yakamuondoa katika kikosi hicho, hadi anasajiliwa na klabu ya Simba, Kapombe hakuwa kwenye timu ya taifa, sijui kigezo gani kilitumika Kapombe akaitwa tena kwenye timu ya taifa na akiwa hajawahi kucheza akiwa na Simba.

Beki huyo aliyeanzia Polisi Morogoro kisha Simba SC na baadaye akaenda nchini Ufaransa kucheza soka la kulipwa ambapo alijiunga na timu ya daraja la nne ya AC Cannes na kurejea Tanzania alikojiunga na Azam FC, Kapombe amejiunga kwa mara nyingine Simba ambapo aliumia mazoezini akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars.

Tangia alipoumia, Kapombe hajarejea tena uwanjani hadi sasa, kauli ya Hanspoppe wala siishangai, ndiyo kauli tunazozisikia kutoka kwq viongozi wetu mbalimbali wakiwemo wa serikali.

Sitamshangaa Hanspoppe, kwa maana hata nakocha wetu wamekuwa wakiingiliwa na viongozi, makocha wamekuwa wakilalamika juu ya kupangiwa vikosi na viongozi na ikitokea kocha amebisha basi anaundiwa zengwe kisha anatimuliwa, viongozi wetu wamekuwq wajuaji kuliko wataalamu husika ambao wao ndio wamesomea taaluma.

Kwa mfano aliyepaswa kueleza ukweli wa suala la Kapombe siyo Hanspoppe bali ni daktari wa timu ambaye ni Yassin Gembe au kocha Omog, lakini anatokea kiongozi asiyejua kitu anabwabwaja, hii ni sawa na ile kauli ya waziri wa Nishati na Madini aliposimama na kusema umeme hautakatika tena na ukikatika itakuwa historia.

Tatizo la kukatika kwa umeme hapa nchini bado limeendelea kuwa tatizo tena kubwa mno, na kama waziri huyo angekaa na wataalamu wanaohusika na masuala ya umeme ambao wanajua tatizo huenda asingekuja na maneno hayo ambayo yanamgharimu hadi sasa, umefika wakati sasa viongozi kuwaachia wataalamu wafanye kazi yao na si kukurupuka kama Hanspoppe kwa Kapombe

Tukutane Ijumaa kwenye Staa Wetu

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA