Kispoti:

WAAMUZI WANAHARIBU UTAMU WA SOKA.

Na Prince Hoza

MCHEZO wa soka ndio unaoongoza kwa kupendwa zaidi hapa duniani, mashabiki wake wamekuwa wengi zaidi kuliko wanaopenda michezo mingineyo kama vile ndondi, riadha, basketiboli, netiboli nk na hiyo ni kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanyika.

Lakini mchezo huo unaharibiwa na watu wachache sana ambao wanatibua utamu wake, kwa mfano pale dunia iliposhuhudia maajabu ya goli la mkono lililofungwa na Diego Maradona kwenye fainali za kombe la dunia.

Maradona alifunga goli hilo dhidi ya timu ya England mwaka 1986 mechi ilikuwa ya Nusu fainali, mwamuzi katika mchezo huo alikuwa Aly Bennoceur raia wa Tunisia ambaye inadaiwa hakuona goli hilo hivyo akapuliza kipyenga kuashiria goli halali.

Achana na goli hilo la Diego Armando Maradona ambalo lilichangia kumpa umaarufu mkubwa duniani, bado mchezo wa soka umeendelea kupendwa duniani kote.

Kwa hapa nyumbani yaani Tanzania mchezo wa soka nao unapendwa na inasadikika ndio unaokamata namba moja, hapa napo kumekuwa na changamoto zake kutoka kwa waamuzi.

Matatizo ya waamuzi yalianza kukera tangu miaka iliyopita na hadi sasa bado hakujapatikana ufumbuzi, kuna maamuzi ambayo yatabaki kwenye kumbukumbu zetu na wala hatutaacha kuzungumza.

Kwa mfano katika mchezo wa fainali ya kombe la Tusker uliofanyika katika uwanja wa Taifa (Sasa Uhuru) jijini Dar es Salaam ilipigwa mbungi kati ya Simba na Yanga, ilikuwa mwanzoni mwa 2000, katika mchezo huo Simba ilishinda mabao 4-1.

Mchezo ulikuwa mzuri na uliudhuriwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, maelfu ya wapenda soka walifurika uwanja wa Taifa kushuhudia mpambano huo wa watani.

Lakini mwamuzi wa mchezo huo Omari Abdulkadir aliharibu utamu wa mchezo baada ya kukubali goli la Madaraka Seleman "Mzee wa kiminyio" ambaye kabla hajafunga aliuseti mpira kwa mkono na kufumua shuti lililotinga wavuni.

Na wakati huo Rais wa klabu ya Yanga, Abbas Tarimba aliwaamuru wachezaji wake kutoka, mashabiki wa Yanga nao waliamua kurusha chupa za maji kwenye meza kuu aliyokaa mgeni rasmi Rais mstaafu, Ally Hassan Mwinyi.

Lakini pia waamuzi waliwahi kuharibu utamu hasa kwenye mechi ambazo zimeshika kasi, kwenye miaka ya 2008 Simba na Yanga ziliumana na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 mchezo wa Ligi Kuu bara uwanja wa Taifa Dar es Salaam, lakini mwamuzi wa mchezo huo alikataa goli la waziwazi la Musa Hassan Mgosi wa Simba ambalo alilifunga na hata wachezaji wa Yanga hawakulitilia shaka.

Lakini mwamuzi alilikataa, na kwq bahati nzuri uwanjani kulikuwa na televisheni kubwa iliyokuwa ikirudia matukio, ikaonyesha jinsi goli hilo lilivyoingia, ambapo mwamuzi akajiridhisha na kuamuru mpira uwekwe kati, hivi karibuni waamuzi wamekuwa wavurugaji wakubwa na kuufanya mchezo huo kukosa uhondo..

Mwaka jana katika uwanja wa Taifa, Simba na Yanga zilikutana Oktoba 1,2016/17 mchezo wa Ligi Kuu Bara, ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, mwamuzi Martin Saanya alikubali goli la Amissi Tambwe ambalo nalo linafanana na lile la Madaraka Seleman, Tambwe aliuseti mpira kwa mkono na kufunga..

Wachezaji wa Simba waliligomea goli hilo na kumfuata mwamuzi lakini nahodha Jonas Mkude alikuwa mstari wa mbele kumzonga mwamuzi ndipo alipolambwa kadi nyekundu.

Lakini baadaye Shirikisho la mpira wa miguu nchini, (TFF) ilipitia vema kadi hiyo nyekundu ya Mkude na kuamua kuitengua na kumfanya Mkude arejee uwanjani, hapo utaona jinsi waamuzi wanavyovuruga uhondo wa soka.

Mwamuzi Ahmed Kiyumbo toka Dodoma alikubali goli la kuotea la Shiza Kichuya wakati Simba ikiilaza Mbeya City bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika uwanja wa Sokoine, Mbeya, pia mwamuzi Heri Sasii wa Dar es Salaam alikataa kuwapa penalti mbilibza waziwazi ambazo Simba ilistahili kupewa ilipocheza na Yanga.

Matokeo katika mchezo huo yalikuwa sare ya 1-1 mechi ikichezwa Oktoba 28 uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Sasii hakuona mpira alipounawa Kevin Yondan, pia hakuona mpira alipounawa Papy Kabamba Tshishimbi.

Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Sunday Manara alionyeshwa kukerwa na waamuzi kiasi kwamba amekuwa akipendekeza waamuzi watoke nje ya nchi, akiamini waamuzi wa ndani hawawezi kusimamia vema sheria 17 za soka.

Lakini Novemba 12 ya Jumapili iliyopita timu yetu ya taifa, Taifa Stars ilitoka sare ya ugenini ya kufungana bao 1-1 dhidi ya wenyeji wao Benin, chakushangaza goli ka Benin ambalo lilikuwa la kuongoza halikuwa halali.

Mwamuzi aliharibu utamu wa soka baada ya kuamuru mkwaju wa penalti uelekezwe langoni kwa Stars, wakati mpira aliunawa mchezaji wa Benin tena nje ya 18, Benin wakapata bao la utata ambalo kila shabiki aliona, mchezo huo ulikuwa ukionyeshwa na na kituo cha televisheni cha Azam, waamuzi wanaharibu utamu wa soka

Inshallah Mungu akipenda tukutane tena Ijumaa Ijayo katika kona yetu ya Staa Wet

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA