Kevin Sabato atia mchanga kitumbua cha Azam, usiku huu
Na Mrisho Hassan. Dar es Salaam
Klabu bingwa Afrika mashariki kati , Azam FC usiku huu imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu Bara, Mtibwa Sugar mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliomalizika usiku huu katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Mchezo ulikuwa mgumu na mkali huku mashambulizi yakielekezwa kila lango, hadi mapumziko timu zote zilikuwa hazijafungana hata bao, kipindi cha pili Azam walianza kulishambulia lango la Mtibwa na kufanikiwa kupata kona iliyoleta sekeseke langoni mwa Mtibwa.
Dakika ya 56 Azam FC waliandika bao la uongozi lililofungwa na mchezaji wake wa kimataifa raia wa Ghana, Enock Atta Agyei aliyeunganisha pasi ya Mbaraka Yusuf, lakini katika dakika ya 75 Mtibwa Sugar walisawazisha goli hilo kupitia kwa Kevin Sabato "Kiduku".
Kwa matokeo hayo Azam imefikisha pointi 23 ikiendelea kukaa katika nafasi ya pili huku Simba ikiendelea kuongoza ligi hiyo na Mtibwa wakishuka hadi nafasi ya tano kuipisha Singida United iliyo katika nafasi ya nne, endapo Sabato asingefunga goli hilo la kusawazisha, Azam wangepaa kileleni