STAA WETU:
JOHN RAPHAEL BOCCO ANAWEZA KUWA MWIBA KWA YANGA KESHO.
Na Prince Hoza
HAYUPO katika mahesabu ya mchezo wa mahasimu Simba na Yanga unaotazamiwa kufanyika jioni ya kesho mishale ya saa 10:00 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ni mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara ambao unaweza kuamuliwa na matokeo ya aina mbili pekee.
Mwamuzi chipukizi Elly Sasii ameshapangwa kuamua 'Derby' hiyo inayowakutanisha watoto wa Kariakoo, ni mechi ya 98 tangu miamba hiyo ikutane katika historia yao, lakini ni mechi ya nne kwa wakufunzi Mcameroon Joseph Marius Omog wa Simba na Mzambia George Lwandamina wa Yanga.
Na katika mechi hizo zote, Omog ameonekana kuibuka mbabe kwa kufanikiwa kushinda mechi tatu mfululizo huku Lwandamina akitoka kapa, na mchezo wake pekee ambao unaweza kumpa ahueni ni huo wa kesho.
Desemba mwaka jana miamba hiyo ilikutana katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la Mapinduzi iliyofanyika visiwani Zanzibar katika uwanja wa Amaan, na katika mchezo huo Yanga ililala kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya dakika 90 kushindwa kufungana hata bao, yaani 0-0.
Na Aprili mwaka huu, miamba hiyo ilikutana tena katika mchezo wa Ligi Kuu bara na Simba kuibuka mshindi wa mabao 2-1, magoli ya washindi siku hiyo yaliwekwa kimiani na Shiza Kichuya na Laudit Mavugo, wakati lile la Yanga lilifungwa na Simon Msuva, na kwa bahati nzuri, Kichuya na Mavugo bado wapo Simba, ila Msuva yeye kwa sasa yupo Difaa El Jadida ya Morocco kwa maana hiyo 'Derby' ya Kariakoo ameipa kisogo.
Agosti 23 juzi juzi tu watani hao wa soka la Tanzania walikutana tena safari hii katika Ngao ya Jamii ambayo ni kiashirio cha kuanza kwa Ligi Kuu bara 2017/18, mechi ilipigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambao kwa sasa upo katika marekebisho, na katika mchezo huo Simba ilichomoza na ushindi wa mabao 5-4 yaliyopatikana kwa penalti.
Miamba hiyo ilienda suluhu ya 0-0 ndani ya dakika 90, hiyo ndio rekodi fupi ya watani hao wa jadi tangu walipoanza kukutana kuanzia Desemba mwaka jana, lakini mechi hiyo ya kesho inajulikana zaidi kwa mechi ya Emmanuel Okwi na Ibrahim Ajibu.
Na hiyo imekuja kwa sababu nyota hao kila mmoja ndiye anayeibeba klabu yake, mpaka sasa Emmanuel Okwi wa Simba ameshaifungia klabu yake mabao 8 na kuwa kinara wa mabao Ligi Kuu kwa sasa huku klabu yake ikishika usukani wa ligi hiyo kwa kujikusanyia alama 15.
Kwa upande wa Ibrahim Ajibu wa Yanga naye ameshaifungia klabu yake hiyo mabao 5 na akishikilia nafasi ya pili nyuma ya Okwi katika orodha ya vinara wa mabao Ligi Kuu bara, na Yanga nayo inakamata nafasi ya pili nyuma ya Simba katika msimano wa ligi ikiwa na pointi 15 sawa na Simba isipokuwa tofauti yao ipo katika magoli ya kufunga.
Na ndio maana mechi hiyo ya kesho inajulikana kwa jina hilo yaani Okwi vs Ajibu kwa wale wasiojua maana yake, lakini wadadisi wengi wa soka hawataki kuamini hilo, kila mmoja anasema lake, kuna wengine wanaiita mechi hiyo ya Niyonzima na Tshishimbi, ama Niyonzima na Ajibu, hata wengineo wamevuka mipaka kabisa wakisema ni mechi ya Omog na Lwandamina.
Lakini mimi nimeenda mbali kidogo na kusema inaweza kuwa mechi ya John Raphael Bocco maarufu Adebayor, unajua kwanini Bocco, nimetazama vizuri site mila zangu na kumuona jamaa huyo akipafomu vizuri hapo kesho na huenda akainyoosha Yanga, na kama si goli la ushindi ama la kusawazisha.
Kama mkufunzi, Joseph Omog atamwingiza katika kikosi chake hiyo kesho ninaamini Bocco atawainua vitini mashabiki wa Simba, na kwanini nampa sana nafasi Bocco na si mwingine kwani Simba inao wachezaji wengi ambao wanao uwezo mkubwa wa kuamua matokeo, ni kwa sababu Bocco amesahaulika mno.
Mshambuliaji huyo aliyezaliwa Agosti 5, 1989 jijini Dar es Salaam na kuibukia katika timu ya Cosmopolitan pia ya Dar es Salaam ameondolewa katika midomo ya wazungumziaji wa Derby hiyo, hakuna hata shabiki anayemjumuhisha straika huyo kwenye kikosi cha kwanza cha Simba na kwa sababu eti amefunga goli moja tu tangu msimu huu uanze.
Na mchezo wa mpira wa miguu siku zote hauna mwenyeww, timu yoyote kati ya hizo zinaweza kushinda katika mpambano huo, kikubwa ni nani anayeamua matokeo, namkubali sana John Bocco kwa mipira ya roose ball, kama mabeki wa Yanga watazembea kidogo basi kijana huyo aliyejiunga na Azam FC mwaka 2006 na kuisaidia kupanda Ligi Kuu mwaka 2008 anaweza kuwa mwiba kwa Yanga.
Bocco ana rekodi nzuri ya kuifunga Yanga lakini akiwa na Azam FC "Wanalambalamba" timu ambayo aliipa mafanikio makubwa kwa kutwaa nayo mataji mbalimbali, Bocco aliiongoza Azam FC kutwaa mara tatu kombe la Mapinduzi, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara (VPL), na Klabu bingwa Afrika mashariki na kati, (Kombe la Kagame).
Mpaka sasa Azam bado mabingwa wa michuano hiyo, Bocco aliiwezesha timu hiyo kutawala soka la Tanzania takribani misimu minne mfululizo ikiwa sambamba na Yanga SC ambao walikuwa wanabadilishana kiti cha usukani Ligi Kuu bara na ushiriki wao wa michuano ya kimataifa, na kwa bahati nzuri mwakani Bocco ataungana na Simba katika ushiriki wa michuano ya kimataifa, Bocco alisajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Azam FC na amejiunga kwa mkataba wa miaka miwili.
Huyo ndio John Raphael Bocco "Adebayor" mtu ambaye hazungumzwi sana kuelekea 'Derby' ya kesho lakini anaweza kufanya maajabu kama akipangwa, lakini mimi huo ni utashi wangu katika kuandika na wala sijabeti ama kujua kama Wekundu wa Msimbazi wanaweza kuchomoka na ushindi kwani lolote laweza kutokea.
Tuonane juma lijalo