MTIBWA SUGAR KURUDI KILELENI LEO?
Na Ikram Khamees. Morogoro
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara inaendelea tena kwa nyasi za viwanja sita kuwaka moto baada ya juzi na jana kufanyika mechi moja moja, Katika uwanja wa Manungu Complex mjini Morogoro shughuri itakuwa pevu pale Mtibwa Sugar itakapowaalika Singida United.
Mchezo huo licha kwamba utakuwa mgumu lakini rekodi zinaibeba Mtibwa Sugar inayonolewa na mwanasoka wake wa zamani, Zuberi Katwila kuibuka na ushindi na kukamata usukani, Mtibwa ina pointi 15 kwa mechi 7 hivyo ikishinda itafikisha pointi 18 itaziacha Simba, Yanga na Azam zenye pointi 16 kila moja.
Simba na Yanga jana zilishindwa kutambiana Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam baada ya kumaliza dakika 90 zikitoka sare ya 1-1, na juzi Azam FC iliifunga Mbeya City bao 1-0 katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi.
Mechi nyingine tano zitapigwa leo ambapo Majimaji itawaalika Mwadui FC, uwanja wa Majimaji Songea, Kagera Sugar na Ndanda zitaumana Kaitaba pale Bukoba, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting, Sokoine Mbeya, Lipuli FC na Mbao FC, Samora mjini Iringa wakati Njombe Mji FC itakapowaalika Stand United pale Sabasaba Stadium, Njombe