KISPOTI:

KWA HILI SIMBA NA YANGA MMEPATIA AISEE.

Na Prince Hoza

ACHANA na matokeo ya juzi Jumamosi ambapo mahasimu Simba na Yanga waliumana vikali uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kumaliza dakika 90 za mchezo kwa kutoka sare ya kufungana bao 1-1.

Sare hiyo ilitokana kwa magoli ya Shiza Kichuya wa Simba aliyefunga kunako dakika ya 57 na Obrey Chirwa wa Yanga aliyefunga dakika ya 60, timu zote sasa zimefikisha pointi 16 huku Simba ikiongoza na Yanga ikifuatia.

Na hiyo yote imetokana na jana Mtibwa Sugar kushindwa kuchomoza na ushindi dhidi ya Singida United ambapo timu hizo zilitoka suluhu 0-0 mechi ikipigwa uwanja wa Manungu Complex Arena mjini Morogoro.

Sare hiyo imewafanya Mtibwa nao kufikisha pointi 16 lakini utasimama katika nafasi ya tatu kwakuwa imezidiwa mabao ya kufunga na vinara Simba waliofunga magoli 20, Yanga waliofunga magoli 11 na wao wenyewe wana magoli 7 tu.

Na sasa narudi kwenye mada yangu ya leo Jumatatu tulivu wenyewe wanaiita 'Blue Monday', Leo nimeamua kuzipongeza Simba na Yanga hasa viongozi wake kwa kuamua kitu kizuri sana.

Naanza kuwasifu Simba ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwa watu wa kwanza kuanzisha mambo mazuri kisha watani zao Yanga hufuata nyuma yao, klabu ya Simba iliyoanzishwa mwaka 1936 mwaka mmoja baada ya kuanzishwa Yanga inamiliki timu mbili kwa sasa.

Simba Queens majuma kadhaa imepanda hadi Ligi Daraja la kwanza ikiungana na Alliance Queens, hilo ni jambo la kuwapongeza sana kwani kuanzisha timu ya mpira wa miguu kwa wanawake kunasaidia kukuza na kuendeleza mpira huo.

Baada ya Simba kuonekana iko mstari wa mbele kuhakikisha soka la wanawake linakua hapa nchini na kuisimamia kidete timu yake hiyo kupanda daraja, watani zao Yanga nao wakafurahishwa na wenzao na kuamua kuanzisha timu yao ya wanawake.

Kwa maana hiyo Yanga Queens mwakani itashiriki Ligi daraja la pili ama la kwanza, na ushindani unaweza kuamia kwenye soka la wanawake pindi timu hizo zitakapokutana, Akizungumza na waandishi wa habari, katibu mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa sambamba na Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano, Dissmas Ten walisema kwamba Yanga nayo inatangaza kuunda timu ya wanawake.

Hiyo ni fulsa adhimu kwa akina dada wanaocheza soka kujiunga na vilabu hivyo, nguvu kubwa ilizonazo Simba na Yanga bila shaka mchezo wa soka la wanawake utapiga hatua, klabu hizo zinajua kupamba mambo yake, angalia leo hii zinapokutana na Simba na Yanga nchi inasimama kwa muda.

Hizo ndio Simba na Yanga, na ninaamini kabisa uwepo wa timu hizo kwenye soka la wanawake kunazidisha msisimko, najua kabisa dada zangu hasa wale wapenda soka najua watakuwa wanafurahia, ni kweli viongozi wa Simba na Yanga wameanza kuamka.

Kwa maana vilabu hivyo vimesajiliwa kama klabu za michezo na siyo klabu za mpira wa miguu peke yake, kama wameanza na soka la wanawake, Simba na Yanga sasa wageukie michezo mingine kama vile ndondi, netiboli na riadha, zamani klabu ya Simba ilikuwa na timu yake ya mchezo wa ndondi.

Mabondia kama Rashid Matumla "Snake Boy" walipitia klabu hiyo iliyokuwa chini ya mwalimu wa ndondi Habibu Kinyogoli, ndipo Jamal Malinzi alipoanza kujiingiza kwenye mchezo huo kupitia kampuni yake ya DJB Promotions ambayo baadaye ikatikisa hapa nchini.

Matumla na wadogo zake walikuwa katika klabu ya Simba, lakini baadaye klabu hiyo ikaua michezo yote na kusaliwa na soka pekee ambapo ikapoteza maana ya kuitwa Simba SC, Yanga nao walistahili kuwa timu za michezo mingine na kwa ukubwa wao zingeweza kushiriki mashindano makubwa ya ndani na nje ya Tanzania.

Nikiwa kama Mtanzania wa kawaida nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya klabu ya Yanga kuamua kuanzisha timu yao ya soka la wanawake, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea katika soka la wanawake hivyo itakuwa nafasi nyingine ya soka letu kupiga hatua.

Naamini kama vilabu hivyo vikubwa hapa nchini vimeunda timu zao za soka la wanawake, Azam FC nao wanaweza kuiga na kuunda ya kwao, Tanzania Prisons nao wakaunda ya kwao, SingidaUnited nao wakaunda ya kwao hata Mtibwa Sugar na nyinginezo nazo zikaunda za kwao,hapo tutakuwa tumepiga hatua kubwa.

Wafadhili nao ndio wakati wenu wa kujitokeza kuzisaidia klabu hizi kutokana na huanzishwaji wa soka la wanawake, Kama tutaendelea kuendeleza kila aina ya michezo naamini maisha yatakuwa safi, yatakuwa safi kwa sababu vijana wengi watapata ajira kupitia michezo hiyo.

Simba na Yanga nawapongeza sana kwa kuunda timu za soka la wanawake, naamini ligi ijayo itashirikisha Simba na Yanga na siku ya kukutana, ushindani wake utakuwa kama ule unaohusisha wanaume, wenzetu huko majuu hasa Uingereza ambapo macho yetu yamezoea kupatazama, klabu za Manchester United, Liverpool au Arsenal na Chelsea zote hizo zinamiliki timu za soka la wanawake na ushindani wake ni mkubwa kama wanavyokutana na wanaume. Tukutane Ijumaa

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA