Goli la tatu lasababisha kipa wa Simba kufariki dunia
Na Mwandishi Wetu. Dar es Salaam
Goli la tatu na timu ya Changanyikeni dhidi ya Abajalo FC mchezo wa Ligi Daraja la pili (SDL) limesababisha kifo cha aliyekuwa mlinda mlango wa zamani wa CDA ya Dodoma, Sigara na Simba SC zote za Dar es Salaam, Rashid Omary Mahadhi (43).
Kipa huyo ambaye pia kaka wa Habibu Mahadhi na Waziri Mahadhi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo na kwa mujibu wa familia mazishi yanatarajia kufanyika kesho mkoani Tanga na msiba upo Kimara jijini Dar es Salaam.
Taarifa za kifo chake zinasema kwamba, marehemu ambaye ni kocha msaidizi wa Abajalo FC ya Sinza ambayo ilikuwa inacheza na Changanyikeni mchezo wa Ligi Daraja la pili, ambapo timu yake ililalakwa mabao 3-0.
Wakati timu yake ikifungwa goli la tatu,hali yake kiafya ilibadilika ghafla na ikabidi apelekwe katika hospitali ya Palestina iliyopo Sinza ambapo mauti yalimfika saa 7 usiku.
Kipa huyo wa zamani wa Simba, ni mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Simba, Omary Mahadhi bin Jabir, marehemu ameacha mke na mtoto mmoja anayeitwa Mahadhi.