STAA WETU:

AZISHI SIMON PETRO: KIPA ALIYEMKIMBIA JUMA KASEJA MBEYA CITY, AFUNGUKA MAKUBWA.
Na Prince Hoza
UNAJUA unaweza usiamini lakini ndiyo ulivyo ukweli, kuwa mlinda mlango Azishi Simon Petro aliikacha Mbeya City mara baada ya kusajiliwa kipa mkongwe aliyepata kuzichezea Simba na Yanga, Juma Kaseja.
Unajua ilikuwa hivi, Azishi alisajiliwa na Mbeya City kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Kimondo FC nayo ya Mbeya, Azishi ambaye alifanya mahojiano na mwandishi wa makala hii kuwa alilazimika kuondoka Mbeya City kwakuwa hakulipwa mishahara ya miezi mitatu na pesa yake ya ada ya usajili.
Anasema Mbeya City walikuwa wanamzungusha kumlipa fedha zake za usajili ambazo ni shilingi Milioni 5, huku pia wakimpiga danadana kumlipa mshahara wake, lakini akashangaa kuona uongozi wa Mbeya City ukimleta Juma Kaseja ambaye alikuwa amevunjiwa mkataba wake na Yanga, kitendo hicho kilimuuma sana na akaamua kurejea Kimondo FC iliyokuwa Daraja la kwanza.
Huyo ndiye Azishi Simon Petro aliyezaliwa Mdaula, Chalinze mkoani Pwani mwaka 1987 na kuanza elimu ya msingi mwaka 1994 hadi mwaka 2001, Azishi anasema alianza kucheza soka tangu anasoma darasa la kwanza.
Anadai kuwa hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari hivyo akaamua kujikita moja kwa moja kwenye mchezo huo akianzia kucheza kama mshambuliaji wa kati (Striker).
Azishi aliamua kuwa golikipa baada ya timu yake ya Mdaula United aliyoanza kuichezea kukosa mlinda mlango wakati wa mechi baada ya aliyekuwa kipa wao kuumia, hivyo akaamua kwenda kukaa langoni na kufanikiwa kuokoa michomo ya washambuliaji wa timu pinzani na kumfanya aanze kuaminiwa.
Uwezo wa Azishi ulionekana mkubwa kuliko kipa wao wa mwanzo na hapo ndipo alipofungua milango ya kusimama katika milingoti miwili ya lango.
AZISHI SIMON PETRO 

Baada ya kuichezea Mdaula United iliyokuwa ikishiriki ligi Daraja la nne kisha akaisaidia kupanda hadi Daraja la tatu, alisajiliwa na timu ya AirBorne ya Morogoro ambayo nayo ilikuwa Ligi Daraja la tatu, na mwaka 2008 akachukuliwa na Polisi Moro iliyokuwa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azishi alicheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza lakini alidumu msimu mmoja kabla ya kujiunga na Rhino FC pia ya Morogoro ambayo ilikuwa Ligi Daraja la kwanza, mwaka 2010 Azishi alienda AFC ya Arusha iliyokuwa Ligi Kuu ambapo alidumu nayo kwa msimu mmoja pia.

Mwaka 2012 hakucheza mashindano yoyote akijiuguza shingo hivyo alisubiri hadi mwaka 2013 ambapo alijiunga na Kimondo FC ya Mbeya iliyokuwa Ligi Daraja la kwanza, alicheza kwa misimu miwili na kujiunga na Mbeya City ambako alidumu kwa msimu mmoja wa 2015/16.

Anasema changamoto mbalimbali amekutana nazo lakini hakuwahi kumkimbia Juma Kaseja akidai uwezo wake ni sawa na kipa huyo mkongwe, "Tofauti yetu ni kwamba yeye mwenzangu ni mkongwe na ni maarufu kuliko mimi, lakini kiuwezo naona tupo sawa", alisema Azishi ambaye ni baba wa watoto watatu, Frank (14), Jeska (10) na Doris (5).

Anakiri kuwa mpaka sasa mwanaye Frank ameanza kufuata nyayo zake kwani naye ni mlinda mlango, Azishi anayevutiwa na Farouk Ramadhan, Mohamed Mwameja na Steven Nemes anasema yeye ni mtoto wa pili kuzaliwa kwa upande wa mama yake.

Kwa sasa Azishi amerejea katika timu yake ya zamani ya Mdaula United inayoshiriki Ligi Daraja la tatu wilayani Bagamoyo, lakini amedai yupo mbioni kujiunga na moja ya vilabu vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hasa baada ya kuachana mazima na Mbeya City.

Kipa huyo aliishitaki Mbeya City kwa Sputanza ili aweze kulipwa haki yake lakini chama hicho kinachoongozwa na mchezaji wa zamani wa Asante Tololi, Musa Kisock kimeshindwa kumsaidia kwani bado hajalipwa chake ingawa amedai akiona kimya atamfuata waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni Dk Harrison Mwakyembe ili kuwasilisha malalamiko
AZISHI SIMON PETRO (KUSHOTO) AKIWA NA MWANDISHI WA MAKALA HII

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA