STAA WETU:
ABBAS PIRA: MTANZANIA ANAYECHEZA SOKA ENGLAND, MAYANGA AMTUPIA MACHO.
Na Prince Hoza.
INAWEZEKANA mafanikio ya Mtanzania Mbwana Ally Samatta yamekuwa kichocheo cha Watanzania wengine wanaocheza nje ya nchi kurejea nyumbani huku wakiwa na shauku kubwa ya kutaka kukipiga kwenye timu yao ya taifa.
Tatizo hapa ni profile zao kutokuwa wazi hususani wale waliondoka Tanzania wakiwa vijana wadogo, Abbas Pira ni Mtanzania mzaliwa wa barabara ya tatu jijini Tanga, Mtoto wa tajiri anayemiliki visima vya mafuta jijini humo, Gulam Pira.
Abbas Pira ni mchezaji wa zamani wa Coastal Union msimu wa 2002/03 na 2004 akiwa chini ya aliyekuwa kocha mkuu wakati huo marehemu Zakaria Kinanda "Sacchi".
Pira aliondoka Tanzania msimu wa mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 17 na kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya masomo ya juu, Akiwa London, Uingereza Abbas Pira, aliendelea kucheza soka kwenye mitaa mbalimbali ya jiji hilo.
Akiwa huko alicheza vilabu kama Hillington FC, FC Wibledon pamoja na Kilbum FC, baadaye Pira alijiunga na kituo cha kukuza vipaji cha Football CV Academy kilichopo kwenye mji wa Northmpton kisha baadaye kwenda kufanya majaribio katika klabu za Chelsea, Birmingham City na MK Dons.
Abbas Pira ni mlinda mlango ambaye alianzia harakati zake za kucheza soka katika timu ya Mzambarauni Stars kabla ajasajiliwa na Coastal Union ambao walianza naye kwa kufanya mazoezi.
Mwaka 2005/06 alienda Uingereza ambako alianza kucheza soka katika vilabu kadhaa, Akiwa Football CV Academy, Pira amesema alicheza pamoja na nahodha msaidizi wa Manchester United Chriss Smalling ambapo anadai alicheza vizuri mpaka akapelekwa kujaribiwa Chelsea.
Alifanya majaribio pale Chelsea kwenye Uwanja wa Stamford Bridge halafu akaenda Birmingham City, Meyton Orient, Coalcheste FC na baada ya hapo alipata ofa ya kwenda MK Dons lakini kulitokea tatizo kwenye kibali cha kazi kwa sababu Tanzania haikuwa ndani ya timu 70 bora kwenye viwango vya FIFA.
Kupata kazi ya mpira Uingereza lazima Tanzania iwe katika nafasi ya 70 kwenye timu bora FIFA.
Pia Abbas Pira amesomea ukocha ambapo amepata leseni C ya UEFA inayomfanya aweze kufundisha timu yoyote ile duniani ya Under-17, Pira pia amekuwa mchambuzi katika vituo kadhaa vya redio hapa nchini.
Anasema amewahi kupigiwa simu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli akimsifia kwa aina yake ya uzungumzaji wake anapochambua, kipa huyo mwenye umbo kubwa anayevutiwa na Zinedine Zidane "Zizzou" na kipa Fabian Barthez, amesema milango imefunguka kwa wachezaji wa Tanzania kucheza soka la kulipwa Ulaya na kwingineko.
Amewasifu Mbwana Samatta, Farid Mussa, Thomas Ulimwengu, Elius Maguli na Simon Msuva kwa kujitoa kwao na kutafuta changamoto nyingine Ughaibuni, amedai bado nafasi zipo kwa wachezaji wa Tanzania kwenda kucheza soka la kulipwa.
Kuhusu kuitwa Taifa Stars. Pira amesema anatamani japo siku moja angalau aitwe kwenye timu ya taifa ii aweze kuibeba vema nchi yake, anasema hivi karibuni alipokea ujumbe kutoka kwa kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga ukimtaka atume profile yake ili iwe rahisi kujumuhishwa kwenye kikosi hicho.
Anaamini uwezo mkubwa anao hivyo atalitetea vema taifa kake, Abbas Pira aliwahi kushawishiwa ajiunge na Simba SC msimu uliopita lakini wakashindwana kwenye dau, yeye alitaka asajiliwe kwa shilingi Milioni 100 za Kitanzania lakini Wekundu hao wa Msimbazi hawakuwa tayari kutoa fedha hizo hivyo alishindwa kujiunga nao.
Abbas Pira kwa sasa anachezea timu ya Wrexham FC inayoshiriki Ligi Daraja la tatu Uingereza na yuko mbioni kwenda nchini Ubelgiji kufanya majaribio katika timu ya Standard Liege inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo